Wanajiolojia watakiwa kuwaelimisha wachimbaji

Madini ya tanzanite


Na Mwandishi Wetu, Arusha

WATAALAMU wa jiolojia nchini wametakiwa kuwaelimisha wachimbaji wa madini ya Tanzanite hususani wachimbaji wadogo mbinu bora na za kisasa za kuendesha uchimbaji.

Aidha wataalamu hao wameelezwa kwa kutoa elimu hiyo kwa wachimbaji, wataweza kuongeza tija, kuzuia uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda usalama wa afya zao na kukuza sekta hiyo ya madini.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Wilaya ya Arumeru Mercy
Silla wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Chama Cha Wajiolojia
Tanzania, ulioanza jana mjini hapa katika hoteli na Naura Spring.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, Silla alisema kuwa Serikali imeandaa na kutekeleza mkakati wa muda mrefu wa kuwasomesha wazawa taaluma mbalimbali ili waweze kusimamia na kuendeleza sekta za madini, maji na nishati.

“Nanawasihi mzingatie wajibu wenu kwa taifa letu mkizingatia Serikali inategemea ushauri na utendaji kazi wenu kwa uadilifu na uzalendo ili kukuza na kuendeleza sekta hizo ambazo ni mhimili mikubwa ya uimarishaji wa uchumi na maendeleo ya jamii hapa nchini,” alisema Silla

Aidha wataalam hao wameshauriwa kuibua mikakati itakayowezesha
kuendeleza taaluma hiyo kwa wazalendo ili kuliwezesha taifa
kujitegemea kwa kuwa na rasilimali watu wenye ujuzi na taaluma ambazo zimejitolesheleza kusimamia na kuendeleza sekta hizo kwa kuwahamasisha washiriki katika kuendesha shughuli hizo.

“Nchi mbalimbali hapa duniani zenye rasilimali, zimeweza kupata
maendeleo makubwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuleta manufaa ya
kijamii kwa wananchi wake kwa kuzitumia vema rasilimali hizo,” alisema

Silla aliongeza kuwa wataalam hao pia wanatakiwa kubuni mikakati
ambayo itawezesha kukabiliana na majanga ya kiasili ya kijiolojia
ikiwemo matetemeko ya ardhi, milipuko ya volkani na gesi chafu ambazo zinatokana na kemikali zinazotoka kwenye miamba na kuchafua mionzi ya asili na maji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wa madini na
nishati nchini Joseph Kahama, aliomba Serikali kwa kushirikiana na
kampuni za madini kuanzisha Chuo Kikuu cha madini, akitolea mfano nchi ya China.

Rais wa Chama hicho Prof. Abdulkarim Mruma alisema lengo la mkutano huo ni pamoja na kujadili mada mbalimbali ikiwemo maendeleo endelevu
katika uvunaji wa madini, nishati na maji ya ardhini.

Profesa huyo alisema kuwa wanahakikisha kuwa faida inayopatikana
kutokana na biashara zao wanawekeza ili kukuza uchumi wa taifa kwa
kuweka mikakati itakayohakikisha wanatumia madini kukuza uchumi. Alisema kupitia mkutano huo watajadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuendeleza sekta ya madini, gesi, mafuta na maji ya ardhini.