JK aongoza maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano


Na Beatrice Mlyansi na Joseph Ishengoma,
Maelezo-Zanzibar

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Kikwete amewaongoza watanzania kwenye maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kitaifa Zanzibar.

Sherehe hizo zilifanyika jana Uwanja wa Amaan Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Rais alipigiwa mizinga 21 kabla ya kukagua gwaride la vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Baadhi ya Viongozi waliohudhuria ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Salmin Amour.

Maadhimisho hayo yalipambwa na halaiki ya watoto 700 kutoka shule za msingi Tanzania bara na Visiwani pamoja na sarakasi kutoka kwa watoto 26 wa shule ya Kimataifa ya Hazina iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na bendi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Kauli mbiu ya Muungano ya mwaka huu inasema “Tudumishe Muungano matunda ya miaka 47 ya Mapinduzi na miaka 50 ya uhuru. “Tumefurahi kuona sherehe hizi zinafanyika Zanzibar mwaka huu kwa sababu zitazidi kuimarisha Muungano”. Alisema Mtumwa Mbarook mkazi wa Mikunguni Zanzibar.

Aidha Mtumwa alishauri viongozi waongeze nguvu kutafuta suluhu ya kero ambazo hazijapatiwa ufumbuzi ili kuleta maana na kuimarisha Muungano.