Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa Tanzania itagharamia ujenzi wa makao makuu ya kudumu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika – African Court on Human and Peoples Rights (ACHPR) mjini Arusha.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inaunga mkono mageuzi yanayokusudiwa kufanywa kwenye muundo wa Mahakama hiyo ili kuiwezesha Mahakama hiyo kuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuzitolewa maamuzi kesi za makosa ya jinai sawa na mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya mjini The Hague, Uholanzi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumanne, Januari 31, 2012 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Majaji wa Mahakama hiyo ya ACHPR wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Gerald Niyungeko kwenye Hoteli ya Sheraton, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Rais Kikwete alikuwa Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika usiku wa jana, Jumatatu, Januari 30, 2012.
Majaji wengine walioambana na Jaji Niyungeko kukutana na Rais Kikwete ni Jaji Sophia Akuffo ambaye ni Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Elsie Nwanuri na Msajili wa Mahakama hiyo Dr. Robert Eno.
Rais Kikwete amewaambia Majaji hao kuwa ni vyema wakati wanafanya maandalizi ya michoro ya jengo la makao makuu ya Mahakama hiyo wakumbuke kuwa hiyo itakuwa ni Mahakama ya Bara zima na wala siyo ya Tanzania na hivyo wafikirie jengo zuri na lenye hadhi inayostahili Mahakama ya Bara la Afrika.
“Kwa kweli tunataka kujenga jengo kubwa na zuri la kuwa makao makuu ya Mahakama yetu hii. Tunataka kujenga Mahakama ya Afrika. Kwa hiyo katika michoro yenu zingatieni jambo hilo kwa sababu tunataka jengo la hadhi,” Rais Kikwete amewaambia Majaji hao.
Ameongeza: “Nyie hangaikeni na michoro mizuri kwa ajili ya jengo lenye hadhi. Habari za fedha za kujenga jengo hilo tuachieni sisi katika Serikali kuona tutafanya vipi.”
Rais pia ameahidi kuwa Serikali itaongeza kasi ya kutafuta ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo mjini Arusha. Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU uliomalizika jana umebariki makao makuu ya Mahakama hiyo kuwa mjini Arusha.
Jaji Niyungeko ametumia fursa hiyo kumweleza Mheshimiwa Rais kuhusu shughuli za Mahakama hiyo na kuishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono shughuli za Mahakama hiyo.
Jaji amemweleza Rais Kikwete kuwa Mahakama hiyo sasa imeanza kupokea kesi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo. Amesema kuwa mwaka jana peke yake, Mahakama hiyo ilipokea kesi 14, ikiwamo moja kutoka Tanzania, na maombi mawili ya kuitaka Mahakama hiyo kutoa ushauri wa kisheria. Amesema kuwa kati ya kesi hizo, tayari kesi saba zilikwishakuamuliwa.
Jaji ameishukuru Tanzania kwa kuunga mkono shughuli za Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mapendekezo ya kuinua hadhi ya Majaji na kubadilisha muundo wa Mahakama hiyo ambao umepanua nafasi za ajira kwenye Mahakama hiyo kwa nafasi 44.