Na Mwandishi Wetu, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha inatarajia kutoa uamuzi wa pingamizi za awali katika kesi iliyofunguliwa na waliokuwa madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaopinga kufukuzwa uanachama.
Pingamizi hizo ambazo zilikuwa zisikilizwe jana, zimekwama baada ya
mawakili kuchelewa kufika mahakamani majira ya saa 2:30 asubuhi. Mbele ya Jaji Fatuma Massengi, mawakili hao walichelewa kutokana na muda uliopangwa kusikiliza pingamizi hizo kubadilishwa na mahakama
juzi. Ilielezwa kuwa muda ulioamriwa na mahakama kusikiliza pingamizi ni saa 2:30 asubuhi.
Jaji Massengi aliwapa muda mawakili wa pande zote kuwasilisha
pingamizi zao kimaandishi ili mahakama iweze kupata muda wa kutosha
kuzipitia pingamizi hizo na kuzitolea maamuzi. Awali Jaji huyo alimuonya vikali Mwanasheria wa Manispaa ya Arusha Lilian Kassanga, kutokana na kushindwa kuwasilisha hati ya kiapo mahakamani hapo.
Mwanasheria huyoa aliieleza mahakama kuwa alishindwa kuandika hati ya kiapo mapema na kuiwasalisha mahakamani hapo mapema kutokana matatizo yaliyokuwa yanamkabili ambayo hakuyafafanua mahakamani hapo, na kuiomba mahakama kumpa siku 7.
“Mara ya mwisho kesi kutajwa hukuwepo mahakamani na leo umeshindwa kuwasilisha hati ya kiapo, inaonesha dhahiri haupo makini halafu unataka nikuongezee muda, are you serious?
“Changamka unaweza ikatokea siku moja ukateuliwa kuwa jaji, utawezaje kufanya kazi katika hali kama hii, kama hati ya kiapo tu inakuchukua muda mrefu kuiandika na kuiwasilisha, kama ndivyo utakwenda hivyo utalemaa,” alihoji Jaji fatuma.
Kwa upande wake wakili wa Chadema, Method Kimomogolo,aliiomba mahakama kuendelea kusikiliza pingamizi za awali zilizowasilishwa.
Hata hivyo Jaji alikubaliana na mawakili hao kuwa Februari 10
Kimomogolo atawasilisha maelezo kimaandishi, Wakili wa walalamikaji
sereviro Lawena februari 17 wakati Lilian akitakiwa kuiwasilisha
Machi 28 mwaka huu au kabla ya tarehe hiyo
Jaji Massengi aliahirisha shauri hilo hadi machi 28 ambapo mahakama
itatoa uamuzi wa pingamizi hizo za awali. Awali Januari 27 mwaka huu pingamizi hizo za awali zilikwama kusikilizwa kutokana na Mwanasheria huyo wa Manispaa kutokufika mahakamani.
Pingamizi hizo zilizowasilishwa na Kimomogolo ni kudai kuwa sheria
iliyotumika kufungua maombi ya kuiomba mahakama kuweka pingamizi kwa Mkurugenzi wa Manispaa kutoitisha uchaguzi na kukitaka Chama
kuwatambua kuwa, haujafuata matakwa ya sheria.
Kimomogolo alidai kuwa sheria hiyo haikufuata matakwa ya sheria kwa
sababu wakati shauri hilo linatolewa hukumu katika Mahakama ya Wilaya ambayo haikuwa na uwezo wa kutolea maamuzi shauri hilo, ambapo iliwaelekeza madiwani hao kukataa rufaa katika Kamati Kuu ya Chadema kabla hawajaenda katika ngazi nyingine ya mahakama.