*Twiga Stars yaingiza mil 38
NAHODHA wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars), Sophia Mwasikili ameondoka Januari 30 mwaka huu kwa ndege ya Turkish Airlines kwenda Uturuki kucheza mpira wa kulipwa.
Mwasikili amekwenda kujiunga na Luleburgazgucu Spor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Wanawake nchini humo. Beki huyo wa kati wa Twiga Stars aliyekuwa akichezea timu ya Sayari Women amejiunga na klabu yake hiyo mpya kwa mkataba wa miaka miwili.
Awali Mwasikili alitakiwa kujiunga mapema na timu hiyo lakini alilazimika kusubiri kwanza mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia (Brave Gladiators) iliyochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, inaripotiwa kuwa mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia (Brave Gladiators) imeingiza sh. 38,220,000.
Kiasi hicho ni kutokana na watazamaji 16,334 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa Januari 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Twiga Stars kuibuka na ushindi wa mabao 5-2.
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 1,000 (watoto), sh. 2,000 (viti vya kijani na bluu), sh. 3,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 5,000 (VIP C na B) na sh. 10,000 kwa VIP A.
Watoto waliokata tiketi kuingia uwanja ni 634, viti vya rangi ya kijani na bluu 13,238, viti vya rangi ya chungwa 1,040, VIP B na C 1,246 na VIP A watazamaji 176.
Vilevile Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki na wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha mechi hiyo kati ya Twiga Stars na Namibia.