CUF yamjibu Hamad Rashid, wenzake 10 mahakamani

Mh. Hamad Rashid

Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) wamewasilisha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam majibu dhidi ya maombi madogo ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake 10 na kuwataka watoe uthibitisho wa madai waliyoyatoa katika maombi hayo. Maombi hayo madogo yamo kwenye kesi ya msingi iliyofunguliwa na Hamad na wenzake hao katika mahakama hiyo.

Katika maombi hayo, Hamad na wenzake hao wanaiomba mahakama hiyo iwaamuru wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kufika mahakamani wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa jela kwa kupuuza amri ya mahakama.

Pia wanaiomba mahakama ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu wa kuwafukuza uanachama na itamke kuwa wao bado ni wanachama halali wa chama hicho. Katika maombi hayo Hamad na wenzake walidai kuwa Baraza Kuu lilikaidi amri ya Mahakama Kuu ya Januari 4, mwaka huu, ambayo iliizuia kuwajadili na kuwasimamisha au kuwafukuza uanachama.

Walidai kuwa CUF ilichukua uamuzi huo hata licha ya kupokea amri hiyo ya mahakama na kwamba, hata wao walipoitwa kujieleza mbele ya baraza hilo kabla ya uamuzi wa kuwafukuza waliionesha amri hiyo ya mahakama, lakini bado baraza hilo likapuuza.

Hata hivyo, wadhamini hao wamekanusha madai hayo kupitia kiapo kinzani  walichokiwasilisha mahakamani jana kupitia kwa wakili wao, Twaha Taslima, wa kampuni ya Uwakili ya Taslima Law Chambers Advocates.

Katika hati ya kiapo kinzani alichokiapa Wakili Taslima mwenyewe kwa niaba ya wadhamini wa CUF, alichokiwasilisha mahakamani jana, wanadai kuwa tuhuma za Hamad na wenzake si za kweli.

Hati hiyo inadai kuwa amri hiyo ya mahakama ilipokewa getini na mlinzi wa ofisi za CUF Makao Makuu aitwaye Selemani Hamad muda wa saa 10.10 jioni. “Wafanyakazi wa wadaiwa isipokuwa mhudumu wa mapokezi, Mize Abubakar Ally walikuwa wameshaondoka kama ilivyo kawaida kuwa hufunga ofisi zao saa 8:00,” inaeleza sehemu ya hati ya kiapo kinzani. Hati hiyo imeambatanishwa na kiapo cha mlinzi huyo na cha mpokea wageni.

Katika maombi yao, Hamad na wenzake wanadai kuwa walipoitwa kujitetea walikataa wakidai kuwa hawezi kufanya hivyo kwa kuwa kuna amri ya mahakama inayolizuia baraza hilo kuendelea kuwajadili na kwamba, waliwaonesha nakala ya amri hiyo.

Hata hivyo, hati hiyo ya kiapo kinzani inadai kuwa Hamad na wenzake walipewa nafasi ya kujitetea na kwamba, baadhi yao waliendelea kujitetea na kusisitiza kuwa hawakupewa kabisa amri hiyo ya mahakama.

Amri ya Mahakama Kuu ya kulizuia Baraza Kuu la CUF ilitolewa Januari 4, mwaka huu na Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza maombi hayo na kesi ya msingi. Maombi ya Hamad na wenzake yaliwasilishwa mahakamani hapo Januari 3, mwaka huu.

Katika maombi hayo, waliiomba mahakama hiyo iamuru mkutano wa Baraza Kuu wa Januari 4, mwaka huu, ambao ulikuwa na lengo la kuwafukuza uanachama, usitishwe hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika.

Katika kesi yao hiyo ya msingi namba 1 ya mwaka 2012, Hamad na wenzake wanahoji uhalali wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya CUF na uteuzi wa wajumbe wake. Kamati hiyo ndio iliyowahoji Hamad na wenzake na kisha kupendekeza kwa Baraza Kuu wafukuzwe au kuwasimamisha uanachama.

 Hata hivyo, licha ya amri hiyo ya Jaji Shangwa, ambayo Hamad na wenzake wanadai kuwa waliiwasilisha mbele ya Baraza hilo kabla ya kufikia uamuzi wa kuwafukuza, CUF iliendelea na kutimiza azma yake ya kuwafukuza uanachama.

Uamuzi huo ndio uliowasukuma Hamad na wenzake kurudi mahakamani kwanza kuijulisha mahakama kuwa CUF imepuuza amri yake na kisha kuiomba mahakama iwaamuru wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa jela kwa kupuuza amri hiyo halali ya mahakama.

Mahakama hiyo imepanga kusikiliza maombi hayo ya Hamad na wenzake Februari 6 na kwamba, hadi kufikia Machi 15, mwaka huu, uamuzi utakuwa umeshatolewa na kesi yote itakuwa imekwisha.

CHANZO: NIPASHE