*Ni wa fani ya upasuaji moyo
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Sudan imesema iko tayari kuleta madaktari ili wasaidie kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania hasa kwenye fani ya upasuaji wa moyo (Open Heart Surgery).
Hayo yamesemwa leo Januari 27, 2012 na Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Dk. Yassir Mohamed Ali wakati alipofika kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Balozi huyo alimweleza Waziri Mkuu kwamba wamekwishaanza mazungumzo na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kuona utekelezaji wa suala hilo. Alisema pia wanaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Kitanzania kwenye eneo la uzalishaji nishati na umeme.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi huyo na kumuahidi kufuatilia suala la uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission-JPC) ili maamuzi yanayofikiwa yaweze kuwa na mfumo maalum wa ufuatiliaji. Aliiomba nchi hiyo iisaidie Tanzania kufundisha pia wataalamu wa kilimo cha umwagiliaji maji kama njia ya kuinua uzalishaji wa mazao nchini.
Alimweleza Balozi huyo kwamba akiwa Arusha wiki iliyopita, alibaini kuwa Chuo cha Ufundi Arushs (ATC) kinakabiliwa na wakufunzi na wataalamu na akaiomba nchi hiyo isaidie kufundisha mafundi sanifu wa umwagiliaji (irrigation technicians) kwa vile imebobea kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa muda mrefu sana.
Mapema leo, Waziri Mkuu alikutana na Balozi mpya wa Japan, Bw. Masaki Okada na kujadiliana naye masuala mbalimbali yakiwemo ya uendelezaji kilimo, miundombinu na miradi ya maji.
Aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuwatuma wakufunzi wawili kwenye Chuo cha Ufundi cha Arusha lakini akatumia fursa hiyo kuomba wataalamu zaidi ili wasaidie kuongeza idadi ya kada ya chini ya wataalamu wa miundimbinu ya umwagiliaji.
“Tunataka kuongeza idadi ya watalaamu wa kilimo cha umwagiliaji maji hasa mafundi sanifu kwa sababu ndiyo wanaohitajika kujenga miundombinu ya umwagiliaji…tumedhamiria kuinua kilimo chetu na hatuna budi kuandaa wataalamu wa kutosha,” alisema.
Aliishukuru Serikali ya Japan kwa misaada ambayo imeipatia Tanzania kwa kipindi chote cha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.