Na Mwandishi Maalumu, Davos-Switzerland
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, David Cameron ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa mfano bora katika kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta za Kilimo na Elimu barani Afrika.
David Cameron ametoa pongezi hizo kwa Rais Jakaya Kikwete wakati wa mazungumzo yao hapa Davos, ambapo wote wawili wanahudhuria mkutano wa Kiuchumi Duniani wa kila mwaka, maarufu kama World Economic Forum (WEF).
Katika mkutano huu wa masuala ya uchumi, pia jitihada anuai zinafanywa ili kukabiliana na athari zinazokabili uchumi duniani kwa sasa na hatimaye kunusuru uchumi huo na njia za kuleta mabadiliko chanya ya kukuza uchumi barani Afrika yanajadiliwa.
“Afrika inapitia kipindi cha mabadiliko ambayo ni chanya, na Tanzania ni mfano bora wa kuigwa katika hili,” alisema Cameron katika mazungumzo na Rais Kikwete.
Katika mazungumzo yao Rais Kikwete amemueleza Cameron kuwa kilimo ni sekta kubwa na inayotegemewa na Watanzania wengi na kwamba serikali inalenga katika kukuza kilimo kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula ndani na nje ya nchi. Rais Kikwete na Cameron pia wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu siasa na usalama barani Afrika.
Mapema jana asubuhi, Rais Kikwete amejumuika na viongozi wengine kutoka Ethiopia, Guinea-Conackry, Kenya na Afrika Kusini kuzungumzia mabadiliko mbalimbali ya uchumi na maendeleo barani Afrika.
Katika mjadala huo uliongozwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Gordon Brown, Rais Kikwete amesema pamoja na mabadiliko hayo, bara la Afrika nalo ni sehemu ya Dunia Uchumi, hivyo nayo kupata athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko hayo ya Kiuchumi duniani.
Rais amesema pamoja na athari na mabadiliko ya Kiuchumi duniani, bado Afrika ina mahitaji zaidi katika kutekeleza sera zinazolenga katika uchumi imara na kuwekeza zaidi katika sekta za elimu, utafiti, kilimo, viwanda na miundombinu.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Bill Gates, pamoja na viongozi wa Ethiopia na Kenya ambapo wamezungumzia namna ambayo, Gates atatoa mchango wake zaidi katika masuala ya kilimo na utafiti.
Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mama Sadako Ogata Rais wa Shirika la Misaada la Japan, maarufu kama Japan International Cooperation Agency (JICA) ambaye naye ameelezea kuwa JICA itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania pamoja na kwamba yeye amefikia kipindi chakustaafu.
Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodafone, Vittorio Colao ambaye ameonesha nia ya kusaidia Tanzania katika kutoa na kusambaza elimu kwa kutumia simu za mkononi katika masuala mbalimbali ya afya, kilimo na elimu.