Slaa awalipua Malecela, Mangula, Magufuli

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa amekoleza moto wa vita ya ufisadi kwa kuibua tuhuma mpya dhidi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Waliotajwa wapya ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Philip Mangula na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.

Dk. Slaa alitoa orodha hiyo mpya jana kwenye uwanja wa Chipukizi mkoani Tabora, wakati akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria katika mkutano wake wa hadhara.
“Nawaambia ndugu zangu kwamba, Mangula na Malecela hawa ni mafisadi ambao leo (jana) tumeamua kuwataja ili watambue, waliohusika moja kwa moja katika sakata zima la wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA),
…Mangula alikuwa akipeleka vimemo kwa wakubwa wake vinavyoonyesha kuidhinishwa kwa ajili ya kuchukua fedha hizo,”alisema Dk. Slaa.
Alisema Malecela wakati huo, akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, alikuwa mshirika wa karibu wa kupanga mikakati ya kufanikisha ukwapuaji wa fedha hizo.
Dk Slaa alisema Magufuli alihusika katika ufisadi wa kuuza nyumba za Serikali alipokuwa waziri katika Serikali ya awamu ya tatu.
Mbali na hayo Dk. Slaa pia alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuueleza umma mahala zilipo zaidi ya Sh bilioni 70 zilizorudishwa na wezi wa EPA .
“Tunataka Rais Kikwete aueleza umma fedha hizi zimepelekwa wapi, kwa sababu hata kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hazioonekani hata senti,”alisema Dk. Slaa.
Kutokana na hali hiyo, ametoa siku 90 kwa serikali kutoa majibu ya kina, vinginevyo Chadema itachukua hatua zinazostahili.
Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, Fred Mpendazoe, alisema mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayotokea duniani, yameonekana kuitia kiwewe CCM.
“Nawaambia upepo huu wa mabadiliko ya kisiasa duniani umewatia kiwewe CCM ile mbaya, wasitarajie hata mabadiliko ya Katiba mpya yatawapa nafuu,”alisema Mpendazoe.
Aliwataka wananchi kuwa makini na CCM, licha ya kujitangaza kuwa imejivua gamba akisema kuwa huo ni ujanja.
Naye kada mpya wa chama hicho Profesa Abdallah Safari, aliwaambia wananchi hao, sera ya udini inayopigiwa kelele kila siku ni ujanja wa CCM, kutaka kuwagawa Watanzania kama ilivyokuwa enzi za utawala wa wakoloni.
“Kuweni makini kumekuwa na tabia watu kutumia udini kutaka kutugawa kwa udini, huu ni ujanja tu kama ule uliyotumiwa na wakoloni kututawala enzi hizo… watataka kutugawa Chadema ili wapate nafasi ya kutuvuruga,”alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake, mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando alisema ofisi yake inaushahidi wa kutosha wa majina ya watu waliohusika na wizi wa fedha za EPA.
Itakumbukwa Septemba 15, 2007 akiwa katika Viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam Dk Slaa aliwataja vigogo 11 wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.

Watu hao ni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Dk.Daud Balali, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Basil Mramba, aliyekuwa Katibu Mkuu (HAZINA), Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Mbunge wa Musoma wa Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), Mbunge Igunga, Rostam Aziz (CCM), mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa.
Mwisho

…Nape: awataka wafungashe virago
*Atuhumu wapinzani kumchafua JK

Na Gabriel Mushi

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amewataka watuhumiwa wengine wa ufisadi waliobakia ndani ya chama hicho kujiuzulu wenyewe kabla hawajawajibishwa.
Nape alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Manzese Jijini Dar es Salaam katika mapokezi ya kuipongeza Sekreatarieti mpya ya chama chake iliyochaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma.
Nape alisema wapo baadhi ya vigogo ambao hawataki kuondoka wenyewe na wameanzisha kampeni chafu za kumchafua Rais, Jakaya Kikwete.
“Sababu tunayo, ari tunayo na nguvu ya kuwaondoa na kushinda vita hii… hawawezi kuzuia mafuriko ya mvua kwa mikono,” Nape alitamba.
“Tukiwasikia watakaotajwa Tabora ni wale wale.. tunataka wafungashe virago, tunataka mabadiliko ya kweli haya ni mwanzo tu.”
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati, aliunga mkono kauli hiyo na kuwataka vigogo hao kuachia ngazi kwa heshima zao.
“Tumewapa muda wa miezi mitatu, wale wote ambao hawajajiuzulu waachie ngazi kwa heshima yao, wasipofanya hivyo halmashauri kuu itawawajibisha,” alisema.
“Tutawashughulikia kuanzia kwenye ngazi ya mashina, kata, kitongoji, wilaya na hata mkoa,” Chiligati akaongeza huku akishangiliwa na umati.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Wilson Mukama, Makamu Mkuu wa CCM, Pius Msekwa, alikiri kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya matatizo makubwa kubainika ndani ya chama ikiwamo ufisadi.
“Jogoo akiwika asubuhi, ni ishara kuwa watu waamke waende kazini, vivyo hivyo katika uchaguzi wa mwaka jana tuliona hali ngumu iliyotokea na kusababisha kupoteza viti vya wabunge, madiwani, viti maalum na hata kura za Rais zikapungua,” Msekwa alisema.
“Wakati huo huo ruzuku ikapungua, kwa hiyo hii ni mbiu, ndio maana Rais akaunda kamati ya wataalamu sita wakiongozwa na Mukama ambao waliyabainisha madhaifu yetu.
“Kubwa ilikuwa ni ufisadi uliopo ndani ya vigogo wanaokumbatiwa na chama, makundi yaliyoibuka ndani ya chama na kupoteza imani kwa wanachama.”
Mukama kwa upande wake alisema wamefanya mabadiliko ya kifalsafa na sasa CCM ni timu imara ya kurudisha imani kwa wananchi wote.