Mwanasheria Manispaa akwamisha kesi ya Madiwani CHADEMA

Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa, Dk Willibrod Slaa

Na Janeth Mushi, Arusha

MWANASHERIA wa Manispaa ya Arusha, Lilian Kassanga amekwamisha usikilizwaji wa kesi ya kupinga kufukuzwa uanchama kwa madiwani watano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kushindwa kufika mahakamani.

Kassanga ambaye anamwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha
Estomih Chan’ga, amekwamisha usikilizwaji wa pingamizi hilo lililotolewa na wakili wa CHADEMA, Method Kimomogolo baada ya
kutokuhudhuria mahakamani hapo jana.

Mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Fatuma Masengi
anayesikiliza shauri hilo, Kimomogolo aliwasilisha pingamizi na kudai kuwa sheria iliyotumika kufungua maombi ya kuiomba mahakama kuweka pingamizi kwa Mkurugenzi wa Manispaa kutoitisha uchaguzi na kukitaka Chama kuwatambua kuwa, haujafuata matakwa ya sheria.

Kimomogolo alidai kuwa sheria hiyo haikufuata matakwa ya sheria kwa
sababu wakati shauri hilo linatolewa hukumu katika Mahakama ya Wilaya iliwaelekeza madiwani hao kukataa rufaa katika Kamati Kuu ya CHADEMA kabla hawajakata rufaa mahakama kuu.

Alidai Mahakamani hapo kuwa walalamikaji wamekiuka amri hiyo
iliyotolewa na Mahakama kwani wamekata Rufaa katika Mahakama kuu kabla ya kukata rufaa katika Kamati Kuu ya CHADEMA.

Jaji Masengi aliahirisha kesi hiyo hadi januari 31 mwaka huu ambapo
Mahakama itasikiliza pingamizi zilizowasilishwa na Kimomogolo. Awali Septemba 20 mwaka jana mahakama ilitupitia mbali kesi iliyokuwa imefunguliwa na madiwani hao ambapo alisema kuwa mahakama hiyo haiwezi kuingilia maamuzi ya Kamati Kuu ya (CHADEMA) ambapo chama hicho kimesajiliwa kisheria kama chama cha siasa hivyo maamuzi waliyoyatoa kwenye chama hicho ni sahihi.

Mguruta alidai kuwa Mahakama hiyo haiwezi kukiuka katiba ya chama
hicho pamoja na maamuzi yote yaliyofikiwa huku akinukuu kesi
mbalimbali ziliwahi kuamuliwa na mahakama mbalimbali nchini.
Waliofungua kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Arusha Estomih Mallah, John Bayo, Ruben Ngowi, Charles Mpanda na Rehema Mohamed.

Shauri hilo namba 12 la mwaka 2011, madiwani hao wamefungua kesi ya
kuomba Mahakama kubatilisha maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu ya
Chadema ya kuwavua uanachama pamoja na kuiomba mahakama kutoa amri la zuio la muda kwa Mkurugenzi asitishe uchaguzi mdogo mpaka Mahakama itakaposikiliza kesi ya msingi na kutolea maamuzi.

Wakili anayewawakkilisha wadai hao ni Serevino Lawena ambaye aliiomba mahakama hiyo kutoa amri ya zuio la muda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha Estomih Chang’a, asiitishe uchaguzi hadi mahakama itakapotoa uamuzi juu ya kesi hiyo.