Na Magreth Kinabo – MAELEZO
SERIKALI imesema imefanikiwa kukusanya mapato yanayotokana na kodi mbalimbali kwa zaidi ya asilimia 100 na kukanusha kuwa imekuwa ikilega lega katika ukusanyaji mapato.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akijibu swali kwa waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa siku mbili wa Mazungumzo wa mwaka kuhusu Sera ya Taifa unaoendelea katika hoteli ya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Ufafanuzi huo ulitolewa na Waziri Mkuu Pinda baada ya kuulizwa swali na waandishi habari kuwa Serikali imekuwa ikilegea katika ukusanyaji huo, kama iliyodaiwa katika hotuba ya Asasi za Kiraia(CBO,s) iliyosomwa katika mkutano huo na Audax Rukonge ambaye ni Mwenyekiti wa Policy From kwa niaba ya asasi hizo.
“Si kweli Serikali imekuwa ikilegea kukusanya mapato yatokanayo na kodi. Tumefanikiwa kukusanya mapato ya kodi kwa zaidi ya asilimia 100 katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne iliyopita. Inawezekana ametoa kauli hiyo kwa kuwa hakuwa na twakimu kutoka Wizara ya Fedha. Hivyo angeenda Wizara ya Fedha ili kupata takwimui,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Waziri Mkuu Pinda, alisema ni wa kufanya tathimini ya kuangalia mipango mbalimbali ya maendeleo kuwa imetekelezwa au kufanyika. Aliongeza jitihada zinahitajika katika kuwekeza kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na sekta nyingine za uvuvi na ufugaji nyuki ili kuongeza uzalishaji. Katika mkutano huo pia suala la kupunguza hali ya umasikini ambapo kama asilimia 70 ya Watanzania wanaishi kwenye hali hiyo.
“Kinachohitajika kufanyika nikumwezesha mkulima mdogo kulima kilimo cha kisasa na kuzalisha chakula cha kutosha na cha ziada mpango huu tulishauuanza kinachohitajika sasa ni kuongeza kasi,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa jambo lingine linalohitajika kuangalia upatikanaji wa masoko kwa ajili ya mazao yanayolimwa na mkulima na kuwasukuma ili waweze kuingia katika mfumo wa viwanda kwa kutumia maligahafi wanazozizalisha mfano pamba. Hata hivyo alisema masuala hayo yanahitaji ushirikiano kutoka katika sekta binafsi.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kundi la Washirika wa Maendeleo na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alberic Kacou alisema ni jambo la linalostahili kutambuliwa katika majadiliano ya mkutano huo kwamba Tanzania imekuwa na mwelekeo chanya wa ukuaji wa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita katika kuimarisha utendaji wake kwenye maendeleo ya watu ikilinganisha na nchi nyingine ndiyo inayofanya vema katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema bado changamoto zinazohusiana na kupunguza umasikini, hivyo ni jambo muhimu kwa serikali na washirika wake wa maendeleo wafanye juhudi zaidi ili ukuaji huo makini wa kiuchumi ambao Tanzania nao katika muongo mmoja uliopita ujidhihirishe kwenye viwango vya kupungua kwa umasikini, upatikanaji wa elimiu na huduma za maji na afya bora zaidi.
Kacou aliongeza kuwa utafutaji fedha hapa nyumbani kwa ajili ya maendeleo ya kitaifa unaweza kupanuka katika miongo ijayo hasa Tanzania inavyoanza kufanya upembuzi wa gesi, mafuta na rasilimali nyingine.
Mwakilishi wa sekta binafsi(TPSF) Dk. Gideon Kaunda akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa sekta hiyo, Esther Mkwizu alisema kuna haja ya serikali kutilia mkazo katika kuwaendeleza ujuzi kwa watu mbalimbali ili kuweza kukuza uchumi na kuboresha maendeleo yao.