Ujenzi wa Barabara ya Korogwe-Same kuanza

*Dk. Magufuli, Kilango washuhudia mkataba wa ujenzi

Na Mwandishi Wetu

UJENZI wa sehemu ya barabara kati ya Korogwe kupitia Mkumbara hadi Same yenye urefu wa kilometa 172 sasa utaanza mara moja baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwatafuta wakandarasi, na tayari wametia saini mikataba kwa ajili utekelezaji.

Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli pamoja na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela wameshuhudia utiaji saini mikataba hiyo.

Awali wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi, Patrick Mfugale alielezea kuwa ili kazi hizo ziweze kukamilika mapema ilibidi mradi huo ugawanywe katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza itaanzia Korogwe hadi Mkumbara ikiwa na urefu wa kilometa 72 wakati sehemu ya pili ni kati ya Same na Mkumbara ikiwa na urefu wa kilometa 96.

Katika sehemu ya kwanza inayoanzia Korogwe hadi Mkumbara (km 72) mkandarasi atakayetekeleza kazi hiyo ni M/S Strabag International GmbH ya Ujerumani kwa gharama ya Shilingi 62,866,110,284 na anatakiwa kuwa amekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi 30.

Mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya sehemu ya Same hadi Mkumbara (km 96) ni M/S DOTT Services Ltd. kutoka Uganda kwa gharama ya Shilingi 65,129,670,563.82 ambaye kwa mujibu wa mkataba anatakiwa kuwa amekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi 30.

Matengenezo hayo kwa sehemu zote mbili yatahusisha uimarishaji wa msingi wa barabara pamoja na kuweka tabaka la lami ya zege kwa na kuongezwa upana kufikia meta 6.5, huku kingo za barabara zikiwa na upana wa meta 1.5 kwa kila upande.

Mhandisi Mfugale ameeleza kuwa kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ukarabati wa daraja la Mombo, upanuzi wa daraja la treni eneo la Mkomazi pamoja na upanuzi wa maeneo mengine ya barabara yenye kona kali.

Maelezo hayo ya Mtendaji Mkuu wa Tanroads yalifuatiwa na salamu za shukrani kutoka kwa Mbunge wa Same Mashariki Mheshimiwa Anne Kilango Malecela ambaye alibainisha wazi kufurahishwa kwake kwa hatua hiyo iliyofikiwa kwani ujenzi wa sehemu hiyo umekuwa ukizungumzwa kwa miaka mingi bila ya kuona hatua thabiti zilizochukuliwa na kwamba sasa ndoto hiyo hatimaye imetimia. Kilango amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa wanawasimamia vyema makandarasi hao ili watimize yale yote wanayotakiwa kukamilisha kwa mujibu wa mikataba yao.

Waziri wa Ujenzi, Magufuli kwa upande wake alianza kwa kumshukuru Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kufanikisha mradi huu hadi kuweza kufikia hatua ya kusainiwa tayari kwa kuanza kazi rasmi. “Sasa jukumu lililobaki ni utekelezaji wa kazi hii jambo ambayo ndilo wajibu wetu kulisimamia,” alisisitiza Magufuli.

Magufuli alitahadharisha kuwa hatavumilia kuona mradi ambao yeye pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Anne Malecela wameitwa kushuhudia uwekaji saini na baadae mradi huo uishie kuwa na matatizo. Aliongeza kuwa itakuwa ni aibu vile vile kwa kampuni kubwa kama Straberg International GmbH kushindwa kukamilisha kazi hizo kwa wakati kwani mradi wanaoutekeleza wao ni wa kilometa 76 tu ikilinganishwa na uwezo walio nao.

Akizungumzia kuhusu usimamizi wa miradi inayoendelea hapa nchini, Mheshimiwa Magufuli amezipongeza Bodi za Usajili wa Makandarasi na Usajili wa Wahandisi kwa kuendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda nje ya taratibu na wajibu wao na kuzitaka Bodi hizo kuendelea kusimamia sheria zao bila kusita.

“Nitafurahi kuona mmoja wa hawa makandarasi ama anafutiwa usajili au anafungwa endapo atashindwa kutimiza wajibu wake wa ki-mkataba” alitahadharisha zaidi Waziri Magufuli.

Akimalizia Mheshimiwa Magufuli aliwataka wasimamizi na watendaji wa Tanroads kuwa makini katika kazi zao kwani alibainisha kuwa ujenzi wa mradi huu umewezakana kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na zitalipwa na wananchi wote hivyo ni lazima watendaji hao wahakikishe kuwa miradi hiyo inasimamiwa ipasavyo.

Aidha aliwataka Makandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao mengine na hasa pale wanapoajiri kwamba wawalipe vibarua na wafanyakazi watakaoajiriwa stahili zao kama ilivyobainishwa katika mikataba waliosaini na kwa kuzingatia sheria za nchi.