Tamasha la kuvumbua vipaji Dar (Grassroot)

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu na kuvumbua vipaji (Grassroot) kwa shule maalum zilizochaguliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam linaendelea Februari 3 mwaka huu.

Siku hiyo tamasha hilo litafanyika katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi wilayani Temeke kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana. Februari 10 mwaka huu tamasha lingine litafanyika katika Shule ya Msingi Kinyerezi wilayani Ilala.

Watoto (wa kike na kiume) wanaotakiwa kushiriki katika matamasha hayo ambayo yataendelea kila wiki katika shule mbalimbali za Dar es Salaam hadi Agosti 24 mwaka huu ni wa kuanzia umri wa miaka 6 hadi 12.

Matamasha hayo ni mwendelezo wa uzinduzi wa Grassroot katika tamasha (festival) kubwa lililofanyika Desemba 17 mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watoto 1,200 baada ya semina iliyoendeshwa na Mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).