Simba kuchezeshwa na Warundi Kigali

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Simba

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba ya Tanzania na Kiyovu Sport ya Rwanda itakayochezwa jijini Kigali.

Waamuzi hao ni Thierry Nkurinziza atakayekuwa katikati wakati wasaidizi wake ni Jean-Claude Birumushahu na Jean-Marie Hakizimana. Mwamuzi wa akiba atakuwa Hudu Munyemana kutoka Rwanda. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.

Mechi hiyo namba 13 itachezwa Februari 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, na itaanza saa 9.30 kwa saa za Rwanda. Mechi ya marudiano itachezwa Machi 4 mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo; Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi namba 3 ya Ligi ya Mabingwa kati ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Atletico Olympique ya Burundi itakayochezwa kati ya Februari 17, 18 na 19 mwaka huu jijini Kinshasa.

Waamuzi wa mechi hiyo ambao wanatoka Gabon watakuwa Mbourou Roponat, Wilfred Nziengu na David Obamba. Mwamuzi wa akiba kutoka DRC ni Mupemba Nkongolo.

Mechi ya marudiano kwa timu hizo itachezwa kati ya Machi 2, 3 na 4 jijini Bujumbura ambapo Kamishna atakuwa Eugene Katamban kutoka Uganda.