Na Janeth Mushi, Arusha
MGOMO wa madaktari ulioitishwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), nchi nzima umeshindwa kuitikiwa mkoani hapa, baada ya madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mt. Meru kuonekana wakiendelea na kazi kama kawa.
Mwandishi wa habari hizi ametembelea hospitalini hapo na kuwakuta madaktari wakiendelea na kazi tofauti na ilivyotangazwa tangu juzi na Chama cha Madaktari, kuanza mgomo wa kada hiyo muhimu.
Hata hivyo tulipofanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo kwa njia ya simu toka mkoani Morogoro, Dk. Omar Chande, kuhusu mgomo huo, alibainisha kuwa madaktari wote hospitalini hapo wanaendelea na kazi.
“Niliondoka tangu juzi huko Arusha, siku ambayo mgomo ulitangazwa
kuanza, lakini madaktari wangu waliendelea na kazi na hata leo bado wanaendelea na kazi kama kawaida, kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu, Miriam Murtazar aliyempa taarifa hizo,” alisema bosi huyo wa Mt. Meru.
Aidha Dk. Chande aliongeza kuwa baadhi ya madai yaliyotolewa na chama hicho yana msingi lakini hayaendani kwa kila sehemu, ndiyo maana madaktari katika hospitali hiyo wanaendelea na kazi kama kawaida.
Alidai kuwa kila sehemu ina utaratibu wake wa kushughulikia
malalamiko na madai na kwamba kwa upande wao yanashughulikiwa na ngazi husika.