ICC yawatia hatiani Ruto, Uhuru, Muthaura na Sang, ni katika vurugu na mauaji ya Kenya 2007

mmoja wa watuhumiwa waliokutwa na hatia katika kesi ya vurugu na mauaji ya Uchaguzi Mkuu 2007 nchini Kenya, William Ruto akiwa ameziba macho.


*Kosgey na Ali wafutiwa mashtaka
HATIMAYE watuhumiwa wanne kati ya Sita waliofikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wamekutwa na hatia hivyo watakabiliwa na kesi ya mauaji na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika mwaka 2007.

Watuhumiwa hao wanne ni Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, pamoja na Mtangazaji wa Redio, Joshua Arap Sang.

Watuhumiwa hao wamekutwa na hatia leo mchana mjini The Hague, Uholanzi baada ya jopo la majaji chini ya uongozi wa Jaji, Ekaterina Trendafilova kuwasilisha uamuzi wao kwa watuhumiwa baada ya maelezo ya awali ya pande zote.

Watuhumiwa hao wanne sasa watashtakiwa kwa makosa waliofikishwa nayo katika mahakama hiyo chini ya majaji mbalimbali, ambapo utaratibu wa mashtaka utatolewa na Mkuu wa ICC hapo baadaye.

Watuhumiwa wawili ambao wamenusurika katika mashtaka hayo baada ya kuonekana hawajaguswa na mashtaka ni Waziri wa Viwanda, Henry Kosgey, pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Generali Hussein Ali.

Mahakama ya ICC iliendesha kikao mwaka uliopita kusikiliza upande wa mashtaka na pia upande wa utetezi kutathmini ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki watuhumiwa sita ambao walionekana kuhusika katika vurugu na mauaji ya raia nchini Kenya baada ya uchaguzi.

Katika kesi ya kwanza, mawaziri wa zamani William Rutto , Henry Kosgey na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang wanatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, na kuwatesa watu.

Uhalifu huo unadaiwa kutekelezwa dhidi ya wafuasi wa chama cha Rais Kibaki cha Party of National Unity (PNU), katika maeneo kadhaa mkoani Rift Valley. Kwenye kesi ya pili, Kenyatta, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura na aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Hussein Ali wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu, mkiwemo mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, ubakaji na mateso.

Kiongozi wa mashtaka katika ICC, Luis Moreno Ocampo anadai kwamba Kenyatta na wenzake walifadhili na kutekeleza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa chama cha Orange Democratic Party, ODM, chake Waziri Mkuu, Raila Odinga, katika maeneo ya Nakuru na Naivasha mkoani Rift Valley. Watu wasiopungua 1,300 waliuwawa wakati wa ghasia hizo, na wengine zaidi ya 500,000 wakapoteza makazi.