Ligi Kuu ya Vodacom kuanza Jumamosi

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza keshokutwa (Januari 21 mwaka huu) kwa mechi nne. Moro United itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mtibwa Sugar itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.

Nayo Toto Africans itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani na Villa Squad itapambana na Kagera Sugar katika Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.

Januari 22 mwaka huu JKT Ruvu na Polisi Dodoma zitapepetana Uwanja wa Azam Chamazi wakati Januari 22 mwaka huu Dar es Salaam itakuwa na mechi mbili; African Lyon na Azam (Uwanja wa Azam Chamazi) na Simba na Coastal Union (Uwanja wa Taifa).

Ratiba kwa ajili ya waamuzi na makamishna kwa mechi 35 za mwanzo tayari imeshatoka. Waamuzi wa kati 16 wameteuliwa kuchezesha mechi hizo huku watatu wakiwa wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Makamishna ni 28 huku watathmini wa waamuzi (referees assessors) wakiwa kwenye mechi tano. Watathmini hao ni Charles Mchau, Soud Abdi, Emmanuel Chaula, Army Sentimea na Joseph Mapunda.

Wakati huo huo; mpaka sasa hakuna kituo cha televisheni ambacho kimeomba na kushinda tenda ya kuonesha moja kwa moja (live) mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Kwa upande wa vituo vya redio, vyote vimepewa haki ya kutangaza moja kwa moja mechi za ligi hiyo kwa masharti yafuatayo;

Kuitambulisha ligi hiyo kwa jina lake (Ligi Kuu ya Vodacom) wakati wa matangazo hayo ya moja kwa moja, na pia kuweka matangazo ya mdhamini (Vodacom) wakati wakitangaza mechi husika. Hata hivyo, vituo vya redio bado vinaruhusiwa kuendelea kutafuta/kutumia matangazo ya wadhamini wao, lakini ambao si washindani wa kibiashara wa Vodacom.

Kwa upande mwingine, mechi kati ya Toto Africans na African Lyon ambayo kwa mujibu wa ratiba ilikuwa ichezwe Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza haitakuwepo, na sasa itapangiwa tarehe nyingine.

Juzi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilipokea barua kutoka kwa wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba ikieleza kuwa Februari 5 mwaka huu uwanja huo utatumika kwa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo hautaweza kutumika kwa Februari 4, 5 na 6 mwaka huu.