Kilimo Kwanza bado akijamnufaisha mkulima

Na Mwandishi Wetu
Morogoro

DHANA ya Kilimo Kwanza imeshindwa kuwanufaisha wazalishaji wadogo wadogo wanaoishi vijijini kutokana na rasilimali zinazotakiwa kuelekezwa katika maeneo hayo kushindwa kutolewa kwa wakati, tafiti zimebainisha.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Ardhi, Yefred Myenzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye warsha ya changamoto za Kilimo Kwanza kwa wazalishaji wadogo kutoka wilaya za Bagamoyo, Kisarawe, Morogoro Vijijini na Kiteto.

Myenzi alisema utafiti umebaini kuwa elimu ya wananchi kuhusiana na Kilimo Kwanza haijatolewa vya kutosha kutokana na wengi wamekiri elimu hiyo ilitolewa tu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Alitolea mfano wa ununuzi wa matrekta madogo ya kulimia maarufu kama “Power Tiller” ambapo uhamasishwaji umekuwa ukifanywa ni mgumu kutekelezwa kwa wakulima wa jembe la mkono kwani trekta moja limekuwa likiuzwa kati ya sh. milioni saba hadi 12.

Alisema katika nguzo ya tano ya Kilimo Kwanza, inasisitizwa kuwepo kwa mabadiliko ya sheria ya ardhi ili kuwezesha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa dhana hiyo, bila kuainishwa nani atafaidika na ardhi, badala yake wazalishaji wakubwa wenye fursa wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kufaidika.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa uwekezaji katika eneo la fedha kwenye kilimo bado ni mdogo huku wanaopata fursa za mikopo kwenye maeneo yanayotajwa wakiwa si wawekezaji wadogo.

Aidha alitoa wito kwa Serikali na wadau wengine wa kilimo kuhakikisha rasilimali za kutosha zinaelekezwa katika maeneo ya vijijini ili wananchi wa kawaida na wazalishaji wadogo waweze kufaidika sambamba na mfumo wa utoaji mikopo kwa ajili ya kilimo itolewe si tu na mabenki ya biashara, bali na taasisi ndogo ndogo za kifedha maeneo ya vijijini.

“Lakini ardhi imekuwa ikitumiwa kama nyenzo na nguzo muhimu ya kuzalisha kwa wananchi wa vijijini ili kujikimu na kuendesha maisha, hivyo si vema kukimbilia kufanya mabadiliko ya sheria za ardhi kwani kwa kufanya hivyo bado kunazidi kutoa fursa kwa wenye nafasi katika jamii kujipatia ardhi dhidi ya wanaoitumia kama nyenzo ya uzalishaji,” alisema Mkurugenzi huyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Stephen Ruvuga, alisema si vema ardhi kuendelea kutolewa ovyo kwa wawekezaji wakubwa kwa kuamini kuwa maeneo yanayotolewa ni mapori, badala yake kila ardhi imekuwa na matumizi, kama si kuchangia, kuishi au kulima.