Mbowe, Dk Slaa waongezewa mashtaka Arusha

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Na Janeth Mushi, Arusha

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kufanya kusanyiko na maandamano
yasiyo na kibali inayowakabili viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha
Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), imeahirishwa hadi Februari 21,
mwaka huu ambapo washtakiwa watasomewa mashtaka mapya.

Aidha katika kesi hiyo washitakiwa hao walikwua wanakabiliwa kwa
makosa nane ila baada ya hati ya mashitaka kufanyiwa marekebisho
wameongezewa mashitaka hadi kufikia 13, ambayo watasomewa kesi hiyo
itakapotajwa.

Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki aliieleza mahakama jana kuwa upande wa mashitaka umefanya marekebisho ya hati ya mashitaka kama
ilivyoamriwa na mahakama Disemba 20 mwaka jana,baada ya wakili wa
upande wa utetezi kuiomba mahakama kutupitia mbali hati hiyo kwa madai kwua haijakidhi matakwa ya sheria.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha Charles Magessa aliahirisha kesi
hiyo jana, baada ya baadhi ya washtakiwa, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu Mkuu wake, Dk. Wilbrod
Slaa, kutofika mahakamani kwa kile kilichodaiwa na wadhamini wao kuwa washitakiwa walikwenda Dar es Salaama kuhudhuria shughuli za kuuaga mwili wa mbunge mwenzao, Regia Mtema (viti Maalum, Chadema)
aliyefariki dunia kwenye ajali ya gari jumamosi iliyopita.

Watuhumiwa wengine ni pamoja na Mke wa Dk.Slaa Josephine Mshumbusi,
Mbunge wa Moshi Mjini,Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Rombo, Joseph
Selasini, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema.

Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na wenzao, wanaoshitakiwa kwa
kufanya maandamano yasiyo na kibali Januari 5, mwaka juzi na
kusababisha vurugu zisizosababisha watu watatu kufariki dunia na
wengien kujeruhiwa.

Aidha watuhumiwa wengine katika shauri hilo Peter Marua na Mathias
Valerian hawakufika mahakamani hapo wala wadhamini wao bila taarifa
zozote Hakimu Magesa aliwataka watuhumiwa hao shauri hilo
litakapotajwa waieleze mahakama sababu za kushindwa kufika mahakamani.

Wakili wa serikali, Edwin Kakolaki aliiomba mahakama kuwachukulia
hatua washtakiwa hao na wadhamini wao kwa kile alichodai wameidharau
mahakama kwa kutofika bila kutoa taarifa kama sheria inavyoelekeza.

Wakili wa utetezi Method Kimomogolo alipinga maombi ya wakili wa
serikali na kuiomba mahakama kuwapa nafasi watuhumiwa hao kujieleza
mahakamani hapo, kesi itakapotajwa.

Hakimu Magesa alisema kuwa kwa mujibu wa sherai mshtakiwa asipofika
mahakamani, mdhamini wake ana jukumu la kuieleza mahakama sababu za
mshtakiwa kutohudhuria mahakamani, na kudai kuwa mahakama imeona busara kutoa nafasi kwa watuhumiwa hao kufika mahakamani Februari 16 mwaka huu na kueleza sababu za wao wala wadhamini wao kushindwa kufika mahakamani.

Disemba 20 mwaka jana, mahakama iliagiza upande wa jamhuri kurekebisha hati ya mashtaka baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa utetezi, Method Kimomogolo kuwa hati hiyo ilikuwa na makosa ya kisheria.

Katika pingamizi lake, wakili Kimomogolo pia aliiomba mahakama
kutupilia mbali hati hiyo kwa madai kuwa inajichanganya ikiwa ni
pamoja na kuwahusisha baadhi yya washtakiwa kwenye kosa ambalo
hawakutenda.

Mbali na Hakimu Magesa kukubaliana na baadhi ya hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa utetezi, alipingana na ombi la Wakili huyo la kuiomba mahakama hiyo kufuta kesi hiyo na washitakiwa kuachiwa huku na kuieleza mahakama kuwa makosa hayo ya kisheria yanaweza kufanyiwa marekebisho. Hakimu Magesa aliiahirisha hadi Februari 21,kutokana na watuhumiwa wengi kutokuwepo mahakamani hapo ambapo shauri hilo litasikilizwa
mfululizo hadi Machi 3 mwaka huu.