Na Janeth Mushi, Arumeru
KAMPUNI ya Simu za Mkononi Airtel imetoa msaada wa kompyuta nne zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 2.8 kwa shule ya Sekondari ya Mlangarini, wilayani hapa mkoani Arusha.
Akimkabidhi misaada hiyo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, Ofisa Uhusianao wa Airtel nchini, Jane Matinda alisema kuwa kupitia faida wanayopata, wanaitumia kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Faida tunayopata tunaitumia kwa kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, tuna imani komputa hizi zitawasaidia wanafunzi kujifunza kupitia mtandao,” alisema Jane.
Ofisa huyo aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, iwapo watatumia kumputa hizo ipasavyo itawasaidia kufahamu matumizi yake wakiwa katika umri
mdogo, itakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi maofisini.
Aidha shule hiyo ambapo ndipo kulipo maktaba ya wilaya hiyo, akikabidhi misaada hiyo kwa shule hiyo Mbunge huyo alisema kuwa makampuni yanaposaidia sekta ya elimu, yatambue kuwa wanawezesha kizazi kijacho kuwa na watumishi bora.
“Makampuni na taasisi mbalimbali mnapotoa misaada katika sekta ya
elimu, mnawekeza kwa kizazi kijacho ili baadaye tuweze kupata watumishi bora wa baadaye,” alisema mbunge huyo.
Mbunge, Medeye, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba Maendeleo na Makazi, aliwataka wanafunzi hao kutumia njia ya mtandao kujisomea
pamoja na wananchi kuweza kufanya biashara na malipo yake kupitia
mtandao.
Alisema kuwa amefanya mazungumzo na kampuni ya Arusha Art ya mjini
hapa, ili wafunge mtandao “internet” shuleni hapo ili wanafunzi waweze kuutumia kujisomea. Kwa upande wake diwani wa Kata ya Mlangarini Mathias Manga aliishukuru kampuni hiyo na kuahidi kulinda rasilimali hizo ambazo zitaweza kuwasaidia wanafunzi wa kizazi hiki na kijacho na kusimamia kikamilifu msaada huo.
Naye Mkuu wa shule hiyo Isack Palangyo, alisema kuwa pamoja na misaada hiyo shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo nyumba za walimu, na umeme.
“Tunaishukuru Airtel kwa msaada huu ila bado shule inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo umeme kwani kwa hivi sasa tunatumia
jenereta, tunaiomba serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu waweze kutusaidia kupunguza changamoto hizi,” alimalizia Mkuu huyo.