Prof. Tibaijuka aenda UN kudai Ukanda wa Kiuchumi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesafiri kuelekea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani kwa ajili ya kuwasilisha andiko la kudai kuongezewa eneo la ziada nje ya maili 200 za ukanda wa kiuchumi katika bahari ya Hindi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Prof. Tibaijuka amesema eneo hilo linatokana na ongezeko lingine la maili 150 ambapo kutokana na utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali kutoka sekta za Ardhi, Maji, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Sheria na wataalamu wa masuala ya baharini kutoka vyuo vikuu umeonesha kuwa eneo hilo ni la Tanzania.

Prof. Tibaijuka amefafanua kuwa eneo hilo limebainika kuwa mali ya Tanzania kutokana na mito mbalimbali kuhusiana na bahari hivyo rasilimali anuai kama vile madini zinaweza kuchukuliwa maji na kupelekwa baharini.

Hata hivyo, amesema baada ya kuwasilisha andiko hilo Tanzania itakwenda tena Umoja wa Mataifa kutetea andiko hilo mwezi Aprili mwaka huu ambapo baada ya utetezi umoja wa mataifa kamisheni ya masuala ya baharini itafanya uamuzi kuhusu Tanzania kutumia eneo la ziada lililo nje ya ukanda wa kiuchumi. Madai hayo yametokana na makubaliano ya kimataifa juu ya sheria ya bahari ya mwaka 1985 ambapo kazi ya kutafiti eneo hilo ilianza mwaka 2007 na imegharimu serikali ya Tanzania zaidi ya sh. bilioni 5.2.