Na Janeth Mushi, Arusha
HALMASHAURI ya Wilaya ya Arusha imeagizwa kuhakikisha inachapisha nakala za kutosha za Katiba ya nchi ya sasa na kuzitawanya kwa wananchi wake ili waweze kusona na kuelewa kabla ya kushiriki kutoa maoni katika katiba mpya.
Changamoto hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye katika mikutano yake ya hadhara aliyoifanya katika Shule ya Msingi Ngaramtoni na Shule ya Kisongo wilayani Arumeru.
Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, amesema hatua hiyo itawafanya wananchi kuielewa vizuri katiba ya sasa kabla ya wao kuanza kutoa maoni katika mchakato wa Katiba mpya.
Aidha lengo la mikutano hiyo ya hadhara lilikuwa ni kuwaelimisha wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kwenye maandalizi ya uandikwaji wa Katiba Mpya, ambapo alisema kuwa Halmashauri inatakiwa kutoa nakala na kuzisambaza katika vijiji ili wananchi waweze kupitia katiba hiyo na kuielewa.
“Ili muweze kutoa maoni ni lazima muwe mmepitia katiba inayotumika hivi sasa ili muweze kubaini mapungufu yake, kaeni kwenye vikundi, kata hata makanisani ipitieni na muichambue kwani hatuwezi kufanya mabadiliko kabla hamjasoma ya awali,”
“Halmashauri inunue nakala za Katiba itolewe kopi walau kila kijiji kiweze kupata nakala moja, wananchi waweze kuzipata na kwa kupitia vikundi wanaweza kutafuta wataalamu wa sheria ili waweze kuwafafanulia, ila muwe makini msije kuwatafuta watu ambao watawapotosha,” aliongeza Naibu huyo
Aidha katika mikutano hiyo Medeye aliwatoa hofu wananchi kuwa Katiba Mpya bado haijatungwa kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa wengine.
“Bunge halijapitisha Katiba Mpya bali imepitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya watu, baada ya kupitishwa Sheria hiyo wananchi mtapata fursa ya kutoa maoni, hivyo mnapaswa kujitokeza kwa wingi kuchangia maoni yenu pindi tume itakapofika katika maeneo yenu,” alisisitiza Medeye.
Alphayo John ambaye ni mkazi wa Mji mdogo wa Kisongo, akitoa maoni yake katika mkutano huo alidai kuwa katika mabadiliko ya katiba ijayo, Katiba ipunguze madaraka ya Rais kwa madai kuwa ni makubwa.
Medeye aliongoza na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Arusha, Watendaji wa Kata, Madiwani na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Aumeru Joseph Ole Sivoiye na Mwenyekiti wa (UVCCM) wilayani humo Esta Maleko.