Na Janeth Mushi, Arusha
KESI inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (CHADEMA) na wanachama 18 wa chama hicho inatarajiwa kuanza kusikilizwa Februari 7 mwaka huu badaa ya upelelezi wake kukamilika.
Mapema leo mbele ya Hakimu Judith Kamala anayesikiliza shauri hilo, Mwendesha mashtaka wa Serikali, Rose Sulley ameiomba mahakama kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza maelezo ya awali ya kesi hiyo.
Katika shauri hilo washtakiwa wote wanakabiliwa na makosa, huku Lema akikabiliwa na makosa matano. Aidha Wakili anayewatetea watuhumiwa hao, Method Kimomogolo leo hakuweza kufika mahakamani ambapo Lema
aliieleza mahakama kuwa Wakili wao ameshindwa kufika mahakamani kutokana na sababu binafsi, ila taarifa za kesi atazipata.
Aidha Mbunge huyo alimuomba Hakimu, mahakama kuzingatia muda kwa madai kuwa kesi waliambiwa kesi itaanza kusikilizwa saa 3 asubuhi ila imeanza kusikilizwa saa 5.30 asubuhi, jambo alilodai linawapotezea muda mwingi.
“Asubuhi tunasikiliza kesi za madai kwanza na kuzitolea maamuzi ambazo huchukua muda mrefu, suala la muda mahakama inaliangalia kwani siku ambayo kunakuwa na kesi inayowahusu kunakuwa na watu wengi hapa, ndiyo maana tunajaraibu kusikiliza kesi zenu mapema ili kuweza kupungza msongamano katika eneo la Mahakama,” alisema Hakimu Kamala
Kosa la kwanzalinalowakabili watuhumiwa hao ni njama za kutenda kinyume cha sheria ya kifungu nambari 384 na 385 cha kanuni ya adhabu, kosa la pili ni kufanya maandamano kutokea barabara ya mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, zilipo Ofisi za Mbunge Lema.
Kosa la tatu ni la Mbunge Lema ambaye anashtakiwa kuhamasisha watu kutenda kosa, ambapo anadaiwa katika eneo la Clock Tower mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, (OCD), Zuberi Mwombeji, kinyume cha kanuni ya adhabu ya 390 na 35.
Shtaka la nne linalowakabili watuhumiwa wote 19 ni kutotii amri
halali ya OCD, Mwombeji ambapo wanadaiwa kuwa katika eneo la Hoteli ya New Arusha, wote kwa pamoja walijipanga na kukataa amri iliyowataka kutawanyika, kinyume cha kifungu cha 42(2) cha sheria ya polisi.
Shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao ni kufanya kusanyiko la watu lisilo halali, kinyume cha sheria ya polisi cha 45 na kifungu cha 14(1) na kanuni ya adhabu, wakidaiwa kuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya zaidi ya waandamanaji 100 wagoma kutii amri za Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha walipotakiwa kutawanyika.