Dk Shein aipongeza kamati ya Mapinduzi Cup 2012

Mchezo wa Fainali za Mapinduzi Cup kati ya Jamhuri ya Pemba na Azam FC, katika mchezo huo Azam ilishinda 3-1.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameipongeza Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Mapinduzi ‘Mapinduzi Cup 2012’ kwa kufanikisha mashindano hayo makubwa kitaifa.

Dk. Shein ametoa pongezi hizo leo alipokuwatana na Wajumbe wa kamati hiyo, pamoja na wafadhili wakubwa wa mashindano ya mwaka huu ambayo yalifikia kilele Januari 12, 2012 kwa timu ya Azam FC ya Mjini Dar es Salaam kutwaa kombe la michuano hiyo kwa upande wa soka, baada ya kuifunga Jamhuri ya Pemba kwenye mchezo wa fainali.

Dk. Shein ameeleza kwamba mashindano hayo ni makubwa ikizingatiwa maudhui yake ambayo ni kuadhimisha mapinduzi matukufu ya Januari 1964, ambayo yamewakomboa wananchi wa Zanzibar. Kwa upande wa netiboli, timu ya taifa ya Uganda iliibuka mshindi kwa upande wa wanawake na Tanzania ikashika nafasi ya kwanza kwa wanaume.

Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kuwataka Wajumbe wa kamati hiyo kuendelea na kazi kwa kujiandaa mapema kwa michuano ya mapinduzi ya mwakani, pamoja na kujitayarisha kwa mashindano makubwa zaidi ya kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2014.

Rais Dk. Shein aliwashukuru wote waliochangia kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha mashindano hayo, ambapo alisema iwapo kutakuwa na ushirikiano na wananchi kujitolea, maendeleo ya michezo nchini, pamoja na sekta nyengine yatapatikana na kuwataka wananchi kuelewa kuwa mashindano hayo ni yao hivyo kila mmoja ashiriki kuyafanikisha.

Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kudokeza kwamba michezo ni moja ya ajenda kubwa za mikakati ya maendeleo katika mwaka huu 2012, hivyo atakutana na Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar (BTMZ), wachezaji wastaafu, viongozi wa michezombali mbali ili kutafuta njia nzuri ya kufanikisha lengo hilo la Serikali.

Alisema ni lazima juhudi za pamoja zichukuliwe kuhakikisha hadhi ya Zanzibar na wanamichezo wake inarejea katika ramani ya michezo kikanda na kidunia, ambapo Zanzibar ilikuwa na sifa kubwa huko nyuma kiasi cha kuogopewa na wachezaji wake kukodiwa kwa michezo maalum muhimu na klabu za Tanzania Bara.

“Uongozi ni hazina kubwa katika michezo popte ulimwenguni, Zanzibar ilikuwa na sifa kubwa kwa sababu waliokuwa wakiongoza vyama vya michezo mbali mbali huko nyuma kama vile soka, netiboli na hoki walijitolea kuhakikisha michezo wanayoisimamia inapata mafanikio, tena bila ya malipo ni moyo…,” alifafanua Dk. Shein.

Akizungumzia timu za taifa za Zanzibar, ile ya soka ‘Zanzibar Heroes’ na ya netiboli, alisema lengo liwe ni kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati na sio kushiriki mashindano tu.

Pamoja na kuimarishwa michezo ya timu za watoto kama vile mashindano ya ‘juvenile’, Dk. Shein alieleza haja ya kila timu kubwa kuwa na timu ndogo za vijana ili ziweze kuinua vipaji na kuzisaidia timu hizo kupata wachezaji.

Kuhusu kutohudhuria fainali za mashindano ya mapinduzi Cup, Dk. Shein amesema alilazimika kuwapa moyo pia wasanii wengine wa utamaduni usiku huo kwa vile tayari mwaka jana amehudhuria fainali za mapinduzi Cup, ili wanautamaduni nao wasivunjike moyo na kuona wanadharauliwa na hakuna sababu nyengine yoyote.

Mapema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed raza, aliishukuru Serikali kwa kuiunga mkono kwa hali na mali tokea kuzinduliwa kwake hadi inakamilisha michuano hiyo, jambo ambalo linaonesha vipi viongozi wanapenda kuona michezo inaendelea.

Kwa upande mwengine, Raza amemhakikishia Dk.Shein kwamba wafanyabiashara wengi na wananchi wako tayari kusaidia maendeleo ya michezo nchini, pamoja na sekta nyengine ilimradi kuwe na mipango na usimamizi mzuri wa fedha.

Aliipongeza kamati yake kwa umoja na moyo wa kujitolea bila kujali muda wala uchovu, jambo ambalo ameeleza ndilo lililofanikisha michuano hiyo kwa kila timu shiriki kuridhika na maandalizi hayo, pamoja na kutokuwepo madeni yoyote.

Wajumbe wa Kamati hiyo ni Mohammed Raza (Mwenyekiti), Sharifa Khamis (Makamu Mwenyekiti), Khamis Abdulla Said (Katibu) na wajumbe ni Dk.Ali Mwinyikai, Amani Makungu, Ali Khalil Mirza, Nassor Salim Al Jazeera, Issa Mlingoti, Abubakar Bakhresa na Farouk Karim.

Kampuni ambazo zilipewa vyeti vya shukurani na Rais kwa kuchangia zaidi ya shilingi milioni tano kwenye michuano hiyo ni Zanzibar Aviation and Travel (ZAT), Zanzibar Ocean View Hotel, Pemba Misali Beach Hotel, Makampuni ya Bakhressa, Multi-Color Printers, Shirika la Bandari la Zanzibar, Royal Furniture and Decor Ltd, Hassan and Sons, Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na Precision Air.