Na Sixmund Begashe
SHIRIKA la Utafiti wa Dawa Barani Afrika (AMREF), limesema vita dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania itafanikiwa endapo wazazi katika familia watakubali kuwa wazi juu ya masuala ya taarifa juu ya ugonjwa huo.
Changamoto hiyo imetolewa juzi mjini Dar es Salaam na mmoja wa maofisa wa Shirika la AMREF nchini Tanzania, Cayus Marina alipokuwa akizungumza na watumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika maadhimisho ya Siku ya Upimaji wa Virusi vya Ukimwi kwa Hiari kwa watumishi wa wizara hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Marina aliwashauri watumishi hao kuwa wazi kwa familia zao juu ya janga la Ukimwi hasa kwa watoto wao kwani kufanya hivyo ni kuwasaidia uelewa mkubwa juu ya tatizo la Ukimwi kwao.
Aidha alizitolea mfano kuwa nchi zilizo endelea kasi ya maambukizi imekuwa ikipungua tofauti na ilivyo kwa nchi za Afrika kutokana na wazazi wengi katika nchi hizo kutoliweka wazi suala la ugonjwa wa Ukimwi hasa katika familia zao.
Kwa upande wake Serikali ya Tanzania imewahamasisha watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini kujitokeza kwa hihari kupima afya zao ili kila mtumishi atambue afya yake na kuendelea kupambana na maambukizi zidi ya virusi vinavyo sababisha Ukimwi.
Akifafanua zaidi katika hafla hiyo, Mkurungezi Raslimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mrimia Mchomvu ambaye ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, katika kongamano hilo la Siku ya Upimaji wa Virusi vya Ukimwi kwa Hiari kwa Watumishi wa wizara hiyo.
Alisema kuwa wizara itaendelea kumuunga mkono, Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa kwenye uzinduzi wa kampeni za kitaifa ya kupima virusi vya Ukimwi kwa hiari iliyofanyika Julai 14, 2007 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.
Mchovu alizitaja faida ambazo wafanyakazi hao watazipata watakapo jitokeza kupima ni pamoja na wataonekana hawana maambukizi ya virusi vya Ukimwi kupata ushauri wa nasaa utakao wasaidia kuepukana na tabia na vitendo vinavyoweza kuleta maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Hata hivyo amesema watakaogundulika wamepata maambukizi wizara itawapatia huduma zinazo stahili.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi ya Wizara hiyo, Suleiman Mvunye alisema kuwa hii ni mara ya pili kwa wizara kuandaa semina inayo hamasisha watumishi wa wizara kupima afya zao, kwani Desemba 29, 2007 watumishi 117 kati ya 130 wa wizara hiyo walijitokeza kupima na mwaka huu 138 wamepima tena Ukimwi kati ya 148, huku 12 wakitoka nje ya wizari hiyo.