Marehemu Rejia Mtema kuagwa Januari 17

Marehemu Mbunge Rejia Mtema

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rejia Mtema aliyefariki jana kwa ajali ya gari anatarajiwa kuagwa kesho Januari 17 jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kuelekea Ifakara mkoani Morogoro kwa mazishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika (Mb) imeeleza kuwa heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa, Januari 17, 2012.

Gari la Mbunge Rejia Mtema baada ya ajali


Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini (kushoto) akichukua maelezo kwenye gari la Regia Mtema namba T296 BSM baada ya ajali.


Mnyika amesema baada ya kuagwa, marehemu atasafirishwa mpaka Ifakara ambapo maziko yanatarajiwa kufanyika Jumatano, Januari 18, 2012.

“CHADEMA tunaendelea kujumuika na familia ya Regia Mtema, bunge na wapenda demokrasia na maendeleo wote nyumbani kwa baba wa marehemu, eneo la Tabata Chang’ombe. Marehemu Regia Mtema ni nyota iliyotoweka mapema lakini kumbukumbu yake itaendelea kuwepo kwa chama na kwa taifa,” amesema katika taarifa hiyo.

Marehemu Regia Estelatus Mtema aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira, alifariki jana papo hapo eneo la Ruvu Darajani baada ya gari lake aina ya Toyota VX kumshinda na kupinduka.