Wateja Vodacom wachanga mil. 11 kusaidia waathirika wa mafuriko

*Ni kupitia “Red Alert” na Vodacom M-Pesa

KAMPENI iliyoendeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kuchangisha fedha kupitia Red Alert na M-Pesa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko jijini Dar es Salaam imechangisha tena sh. 11,607,470.

Kampeni hiyo iliyodumu kwa wiki tatu kuanzia Disemba 22 mwaka jana hadi Januari 10, 2011 imefanikisha kupatikana fedha hizo zilizochanganywa na wateja kuunga mkono juhudi za Vodacom za kusaidia waathirika wa maafa hayo.

Kampuni ya Vodacom ilitangaza kuwashwa kwa nambari ya Red Alert na kuweka nambari maalum ya kuchangia kwa M-Pesa saa chache baada ya kutolewa taarifa rasmi za kuwepo kwa athari kubwa za mvua zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo Dar es Salaam na kuleta madhara hayo hasa kwa wakazi wa mabondeni.

“Kila mtu alikuwa na nafasi ya kusaidia kuokoa na kusitiri maisha ya wenzetu waliothiriwa na ndio maana tukawasha nambari ya Red Alert na kuruhusu uchangiaji kupitia M-Pesa,” Amesema Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania, Mwamvita Makamba.

Nambari ya Red Alert hutumika na Vodacom wakati wa maafa kuwezesha wateja kuchangia fedha kusaidia waathirika na hakuna makato yanayofanywa katika ujumbe mfupi unaotumwa katika nambari hii ili kiwango kinachopatikana kiwanufaishe waathirika moja kwa moja.

Maafa yaliyotokana na mvua kubwa zilizoonyesha sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Dar es salaam Disemba mwaka jana yaligharimu maisha ya watu huku maelfu ya familia yakiachwa bila makazi.

“Ni jambo la faraja kwamba tumeweza kusimama kama familia moja ya Vodacom. Wafanyakazi, wateja wetu na wadau na kuonesha upendo wetu wa dhati dhidi ya wenzetu waliopatwa na maafa hayo.” Aliongeza Mwamvita.

Kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii – Vodacom Foundation inaandaa utaratibu wa michango hiyo kuwanufaisha walengwa kama ilivyokusudiwa.

Awali Vodacom Tanzania ilichangia vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni thelathini vikiwemo vyakula, magodoro na mablanketi kwa waathirika wa maafa ya Dar es Salaam waliokuwa wakiishi katika kambi maalum kwa wakati huo.

Ujumbe mmoja wa maneno kwenda nambari ya Red Alert 15599 uligharimu Tzs 500/-, na kwenda m-pesa nambari 155990 uligharamu Tzs. 1,000/- na kwamba hakukuwepo na ukomo wa kutuma ujumbe na kuchangia.