RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Januari 11, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mohamed Tamel Amr.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili, masuala ya kikanda na kimataifa.
Waziri Tamel Amr na ujumbe wake walikuwa nchini kwa ziara ya siku moja na waliondoka mara tu baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo na Rais Kikwete.
Viongozi hao wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kufanya mkutano wa wakuu wa nchi zinazotumia maji ya Mto Nile, ili kujadili namna bora zaidi ya kuiwezesha kila nchi unakopitia mto huo kunufaika kwa njia mwafaka na matumizi ya maji ya mto huo bila kuathiri haki ya nchi nyingine katika kutumia maji hayo.
Rais Kikwete amemweleza, Tamel Amr kuhusu juhudi ambazo amefanya binafsi katika kuwashawishi baadhi ya wakuu wa nchi zinazotumia maji ya Mto Nile kukubali kuhudhuria kikao cha wakuu wa nchi hizo ambacho kitaitishwa katika wakati mwafaka na kwenye nchi itakayokubalika.
Naye Waziri Tamel Amr amemwambia Rais Kikwete kuwa ni muhimu kwa nchi ambako unapita Mto Nile kukubaliana kushirikiana katika matumizi ya maji ya mto huo. “Mto huu na maji yake linatakiwa kuwa jambo la kutuunganisha zaidi na siyo kutugawa.”
Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuhusu umuhimu wa Tanzania na Misri kushirikiana katika uwekezaji na hasa katika maeneo ya kilimo na matumizi bora ya maji.
“Kwa hakika kuna maeneo mengi ambako tunaweza kushirikiana na moja ya maeneo hayo ni katika kilimo kwa sababu Misri ni nchi mfano mzuri hasa kwenye kilimo cha mboga na matunda na jinsi ya kutumia maji kidogo kuwawezesha watu kushiriki kilimo cha maana na cha kisasa. Nilipotembelea Misri, nilishuhudia binafsi jinsi maji kidogo yanavyoweza kutumika kufanikisha kilimo cha kisasa hata kwenye jangwa,” Rais amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje huyo.
Ameongeza Rais Kikwete, “Nyie mna uzoefu mkubwa katika kutafuta na kutumia maji chini ya ardhi kwa sababu hili pia ni eneo ambako mmekuwa viongozi.”
Rais Kikwete pia amemweleza Waziri Tamel Amr kuhusu historia ya miaka mingi ya uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Misri tokea enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais Gamal Nasser wa Misri na jinsi katika miaka yote nchi hizo mbili zimesaidiana wakati unakuwepo ulazima wa kusaidiana.