Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Wachina wanaofanya kazi nchini Tanzania imetangaza mwaka mpya wa Kichina ambao shamrashamra za maadhimisho hayo zitafanyika Jumapili ijayo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo, Mkurugenzi wa Masuala ya Habari na Uhusiano wa Jumuiya hiyo, Yang Xiao amesema katika mwaka huu mpya wa kichina, China imedhamiria kuitazama Afrika kama mshirika mkubwa wa maendeleo.
Amesema urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika unatoa fursa ya ushirikiano unaozinufaisha pande zote mbili hususani China na Tanzania ambazo ushirikiano wao ni wa kihistoria.
Xiao ameeleza kuwa ushirikiano kati ya China na Tanzania ni mfano wa kuigwa kwani ushirikiano huo umeboreka zaidi baada ya wakuu wa nchi hizo mbili kutembeleana na kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano baina ya China na Afrika, mkataba uliosainiwa mjini Sharm el Sheikh nchini Misri.
Amebainisha kuwa katika maadhimisho ya mwaka mpya wa China katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jumapili ya wiki hii, kutakuwa na vikundi mbalimbali vya sanaa, vikiwemo vya kutoka nchini China na vya hapa nchini.