Na Magreth Kinabo–Maelezo
SERIKALI imesema kuanzia mwaka huu imerudisha hadhi ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili, hivyo mwanafunzi atakayepata wastani wa chini ya asilimia 30 hata ruhusiwa kuendelea na kidato cha tatu, bali ataruhusiwa kukariri darasa mara moja tu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulugo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu tamko la Serikali la kupandishwa hadhi ya mitihani hiyo na gharama za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Imesema kuwa mwanafunzi atakariri na kushindwa kufikia wastani wa asilimia 30 ataondolewa katika mfumo rasmi wa elimu. Mbali na hilo imesema ina mpango wa kurudisha hadhi mtihani wa darasa la nne, hivyo itatoa maelekezo hapo baadaye baada ya kumalizika kwa uchunguzi.
Aidha imeongeza kuwa wazazi na walezi watapaswa kuchangia gharama za uendeshaji wa mitihani hiyo, ikiwemo mingine ya kitaifa ya kidato cha nne na sita kuanzia mwaka huu. “Kuanzia leo tunarudisha hadhi yake,” alisema Waziri Mulugo.
Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika uchunguzi uliofanyika mwaka jana kubaini kuwa moja ya sababu zilizochangia ufaulu duni wa wanafunzi wa kidato cha nne, mwaka 2010 ni kutokana na kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo hata baada kushindwa kufikia alama ya ufaulu. Uchunguzi Ulifanyika baada ya Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania kuagiza serikali na wadau wengine kufuatilia chanzo cha kushuka kwa ufaulu huo.
Waziri Mulugo alisema ufaulu wa kidato cha pili umekuwa ukishuka kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2010 hivyo kuashiria wanafunzi na walimu kutofanya bidii za makusudi katika kujifunza na kufundisha.
Akizungumzia kuhusu uchangiaji wa elimu wa gharama za uendeshaji wa mitihani ya Taifa alisema uendeshaji wa mtihani umekuwa mgumu kufutia ongezeko la gharama za uendeshaji linaloendana sambamba na ongezeko la idadi ya shule pamoja na wanafunzi mwaka hadi mwaka, ambapo alitolea mfano wa mtihani wa kidato cha pili gharama za zake ni sh. bilioni sita wakati wa kidato cha nne ni sh. bilioni 27.9.
Alisema katika mtihani huo wazazi na walezi watakiwa kuchangia sh. 10,000 kwa kila mwanafunzi kwa shule za serikali na zisizo za serikali.
Kwa upande wa mitihani ya kidato cha nne na sita wazazi na walezi watapaswa kuchangia sh .35,000 kwa kila mwanafunzi kwa shule za serikali na zisizo za serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Mulugo alisema serikali inatarajia kutangaza ajira za walimu wa msingi na sekondari mwezi huu , na hivi karibuni itatangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili.
Hii ni ni mara ya pili kwa serikali kurejesha mtihani wa kidato cha pili mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1999 tangu ulipoanzishwa mwaka 1984.