Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete leo, Jumanne, Januari 10, 2012, amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watano ambao wataziwakilisha nchi zao katika Tanzania.
Katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais amepokea hati za utambulisho wa Balozi wa Denmark, Johnny Flentoe, Balozi wa Malawi, Mama Flossie Asekanao Gomile-Chidyaonga, Balozi wa Umoja wa Ulaya, Filiberto Cerian Sibregondi, Balozi wa Burundi, Issa Ntambuka na Balozi wa Uturuki, Ali Davutoglu.
Katika mazungumzo na Balozi Flontoe wa Denmark, Rais Kikwete ameishukuru nchi hiyo kwa misaada mingi na ya miaka mingi ya maendeleo ambayo nchi hiyo imekuwa inatoa kwa Tanzania. “Tumenufaika sana na uhusiano mzuri baina ya nchi zetu na kiwango cha maendeleo yetu kimechangia vizuri na Denmark,” amesema.
Rais Kikwete na kuongeza: “Tunafurahi pia Tanzania ilikaribishwa kushiriki na kutoa mchango katika Kamisheni ya Afrika iliyoangalia fursa za ajira kwa vijana katika Afrika. Changamoto kubwa kwetu sasa ni namna ya kutengeneza ajira za kutosha kwa maelfu ya vijana wanaomaliza shule kila mwaka kutokana na upanuzi mkubwa wa nafasi za elimu katika Tanzania.”
Rais Kikwete alikuwa Kamishna katika Tume hiyo iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Denmark, Anders Fogh Rasmussen na iliyotoa ripoti yake iitwayo Africa Commission: Realising the Potential of Africa’s Youth mwezi Mei 2009. Katika mazungumzo na Rais Kikwete, balozi mpya wa Malawi, Balozi Gomile-Chidyaonga ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kutoa njia ya Malawi kupitishia bidhaa zake.
“Uchumi wetu katika Malawi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Tanzania kuendelea kuiruhusu Malawi kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kutumia barabara zake kupitishia bidhaa zetu,” amesema mama huyo.
Naye Rais Kikwete amemweleza kuwa: “Nchi zetu zina uhusiano mzuri na wa karibu sana. Watu wetu ni wamoja na tutaendelea kuimarisha uhusiano huo na kushirikiana zaidi. Kama unavyojua, unaweza kuchagua rafiki lakini huwezi kuchagua jirani.”
Katika mazungumzo na Balozi Sibregondi wa Umoja wa Ulaya, Rais Kikwete amezungumzia umuhimu wa jinsi Tanzania na Umoja huo kushirikiana katika kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Kigoma ili kuwezesha Tanzania kuunganishwa kwa barabara ya lami na nchi jirani ya Burundi.
“Tunahitaji kuendelea na ujenzi wa miundombinu na hasa ujenzi wa barabara kati ya Manyoni na Kigoma ili kufungua ushoroba wa magharibi mwa Tanzania.”
Rais Kikwete amemhakikishia Balozi Ntambuka wa Burundi kuwa Tanzania itaendelea kufungua ardhi na njia zake kwa ajili ya kupitishia bidhaa za Burundi. “Burundi ni nchi rafiki, ni nchi jirani, uhusiano wetu ni mzuri na tunashirikiana pia kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki. Nataka kukuhakikishia kuwa Bandari za Tanzania na ardhi yake vitaendelea kuwa wazi kwa matumizi ya Burundi.”
Naye Balozi Ntambuka ameishukuru Tanzania kwa mchango wake wa kutafuta amani katika Burundi. “Hakuna sababu ya kurudia historia, lakini wenyewe tunajua tulipotoka na tunajua waliotusaidia. Bado wachanga, na ni muhimu Tanzania kuendelea kutulea na kutusaidia.”
Rais Kikwete na Balozi Davutoglu wa Uturuki wamekubaliana kuelekeza nguvu zaidi katika kujenga na kukuza uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. “Uhusiano wetu wa kidiplomasia ni mzuri sana, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ndio unaanza. Tunahitaji kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza uhusiano wa kiuchumi,” amesema Rais Kikwete.
Balozi Davutoglu pia ameishukuru Tanzania kwa kutoa ardhi ambako Uturuki itajenga chuo kikuu.