Katiba ya wanachama TFF yarekebishwa

Rais wa TFF, Leodger Tenga

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji pia ilifanyia kazi suala la marekebisho ya katiba za wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Katiba hizo zimegawanywa katika makundi matatu; katiba za wanachama wapya, katiba ambazo tayari zimerekebishwa na katiba ambazo hazijarekebishwa.

Maelekezo ya Kamati ni kuwa itatoa mwelekeo (roadmap) utakaoonesha muda wa mwisho (deadline) wa kufanya marekebisho kwa makundi yote hayo matatu ambapo kwa wanachama watakaoshindwa hawataruhusiwa kuingia kwenye Mkutano Mkuu wa TFF.

Maeneo ya msingi ya marekebisho ni sifa za uongozi. Katiba zote za wanachama wa TFF kwa upande wa sifa za uongozi ni lazima ziwe sawa. Maeneo mengine ni kuainishwa wazi kwa majukumu ya Kamati ya Utendaji, Mkutano Mkuu na namna ya kutatua migogoro ya wanachama ili kuepuka watu kwenda mahakamani.