Hakuna Mzanzibar ambaye hajanufaika na Mapinduzi-Dk Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizindua barabara.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema hakuna mwananchi hata mmoja wa Zanzibar anaweza kusimama na kupinga kuwa hajafaidika na matunda ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Dk. Shein aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa barabara sita Kisiwani Pemba zikiwemo barabara ya Chanjani-Pujini, Chanjamjawiri-Tundauwa na Mtambile-Kangani, Mtambile-Kengeja hadi Mwambe, Mizingani –Wambaa, Kenya – Chambani zilizopo Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni shamra shamra za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein ambaye jana alizindua barabara nne kwa pamoja na leo barabara mbili zilizobaki katika Wilaya ya ChekeChake zilizojengwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Norway kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa wananchi wote wa Zanzibar wamefaidika na Mapinduzi matukufu ya Januari 1964 na hakuna atakaesema kuwa yeye hakufaidika na kusisitiza kuwa kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuyalinda, kuyatunza na kuyaenzi Mapiduzi hayo.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inawajali na inawathamini na inawasiliza wananchi wake na ndio maana inaendeleza juhjudi za kuwawekea mazingira bora ya kimaisha sanjari na kuwapelekea karibu huduma za maendeleo zikiwemo barabara, maji safi na salama, elimu, afya na huduma nyengine za kimaendeleo.

“Sisi wengine tuliopo hapa na wale wasiokuwepo hapa hii leo hakuna hata mmoja anaeweza kusema kuwa hajafaidika na matunda ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwataka wananchi wanapoona uharibifu wa barabara kutoa taarifa kwa Idara ya Barabara ambayo nayo ilitakiwa kutopuuza taarifa za uharibifu huo kwani tabia hiyo imekuweko hata katika Shirika la umeme la kupuuza taarifa za wananchi.

Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa barabara hizo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta za maendeleo na kusisitiza barabara hizo kutunzwa na kuenziwa ili zimewe kutumika hivi sasa na hapo baadae sanjari na kuwataka madereva kutokwenda mwendo wa kasi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kutojenga pembezoni mwa barabara hizo kwani serikali haijafikia ukomo wa ujenzi wa barabara kutokana na idadi ya Wazanzibari kuongezeka ambapo hivi sasa idadi ya Wazanibari inakisiwa kuwa zaidi ya Milioni moja.

Katika maelezo yake katika maeneo yote aliyozindua barabara Dk. Shein hakuchelea kutoa shukurani na pongezi kwa Wizara ya Mawasilaino pamoja na uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume kwa kuanzisha miradi hiyo na kutoa shukurani kwa wananchi kwa kumchagua yeye kuwa Rais kwa lengo la kuyaendeleza pale palipofikiwa.

Dk. Shein alisema kuwa kutokana na juhudi hizo za awamu ya sita awamu yake ya saba itaendeleza miradi hiyo ambayo tayari imeshakamilika sanjari na kuanzisha mipya kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake na kueleza kuwa utaalamu huo utasambaa Zanzibar nzima.

Pia, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Pemba kuwa tokea kuaisisiwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kumekuwa na usawa wa kuimarisha miradi ya maendeleo kati ya Unguja na Pemba.

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa wananchi wote walioshiriki katika ujenzi wa barabara hizo zilizotumia barabara ya lami baridi na kueleza kuwa ushirikiano wao ndio uliozaa matunda na kuleta mafanikio na kussisitiza kuwa penye mashirikiano mara zote maendeleo huimarika.

Naye Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad, alisema kuwa mradi huo wa barabara za vijijini Kusini Pemba zimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Norway kupitia Shirika lake la Norad kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema kuwa barabara hizo zote sita zimejengwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kupitia Idara ya UUB na kusimamiwa na Kampuni ya Pory Infra ya Swizerland ambao uliaza tarehe 1 Januari 2009 na barabara ya mwanzo ilioanza i barabara ya Mtambile-Mwambe.

Waziri Hamad alieleza kuwa barabara hizo zimejengwa kwa aina yake ambapo zilitumia mfumo wa kuwashirikisha wananchi kwa njia ya nguvu kazi bila ya kujali itikadi ya vyama vya siasa na zilitumia teknolojia ya lami baridi ambapo gharama za ujenzi zilizotumika ni Dola za Marekani milini 11.4 zilizotolewa na Norway na serikali ilichangia Dola milioni moja.

Aidha, alieleza kuwa jumla ya wananchi 2085 wakiwemo wanawake 606 na wanaume 1479 walipata ajira na jumla ya sh. 1.2 Bilioni zimerudi kwa wananchi kwa njia ya mishahara na posho na kuweza kuzitumia vizuri katika maendeleo yao. Pia alielezakuwa tayari ujenzi wa barabara 6 za Mkoa wa Kaskazini umeanza rasmi chini ya Kampuni ya ECH Yong.

Mapema Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik, alieleza kuwa mradi huo wa barabara ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu wa kimaendeleo kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Norway na kusifu uongozi wa Dk Shein kwa kuendeleza amani na utulivu nchini.

Alieleza kuwa kuimarika kwa miundombinu ya barabara kutasaidia kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo sekta ya utalii, biashara pamoja na kilimo na kusisitiza kuwa mradi huo wa ujenzi pia, utasaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi.