*Ligi Daraja la Kwanza Bara Feb 4
SIKU za mechi kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ambayo itaanza mzunguko wake wa pili Januari 21 mwaka huu sasa itakuwa ni Jumamosi, Jumapili na Jumatano tu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kupitia kwa Ofisa Habari wake, jana Boniface Wambura imesema uamuzi huo umefanya na Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana Januari 5, 2012; ambapo pamoja na mambo mengine ilikuwa kupitia ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom na ile ya Daraja la Kwanza.
Wambura amesema mabadiliko hayo yanatokana na kituo cha Dar es Salaam kuwa na timu saba kati ya 14 za Ligi Kuu zinazotumia viwanja viwili tu (Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Azam), kamati imepitisha uamuzi kuwa mechi mbili zinaweza kuchezwa kwa wakati mmoja (Taifa na Azam) ili ligi ichezwe ndani ya kalenda.
Timu zinazotumia viwanja hivyo kama vya nyumbani katika Ligi Kuu ya Vodacom ni African Lyon, Azam, JKT Ruvu Stars, Moro United, Villa Squad, Simba na Yanga.
Wakati huo huo, Wambura amesema mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayochezwa katika makundi matatu tofauti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza Februari 4 mwaka huu. Timu zitakazomaliza katika nafasi tatu za juu zitacheza hatua ya fainali itakayokuwa na timu tisa.
“Kundi A lenye timu za Burkina Faso ya Morogoro, Mgambo Shooting ya Tanga, Morani ya Manyara, Polisi ya Dar es Salaam, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam litaanza ligi hiyo kwa mechi moja kati ya Morani na Burkina Faso itakayochezwa mkoani Manyara,” amesema Wambura katika taarifa yake.
Ameongeza kuwa Februari 4 mwaka huu katika kundi B kutakuwa na mechi kati ya Small Kids ya Rukwa na Polisi ya Iringa itakayochezwa mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji na Mlale JKT wataoneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Hata hivyo ametanabaisha kwamba kundi C mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Manyoni FC na AFC itakayofanyika mjini Singida, Rhino FC dhidi ya Polisi ya Tabora zitacheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati 94 KJ na Polisi ya Morogoro zitakwaruzana Februari 5 mwaka huu mjini Mlandizi.