Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
UWEKAJI wa jiwe la msingi nyumba ya madaktari wa Norway ni miongoni mwa hatua za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Saba, za kuenzi na kuendeleza matunda ya Mapinduzi kwa kuziimarisha huduma za afya nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la nyumba ya Madaktari wa Norway, inayojenwga huko katika Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo aliloliwekea jiwe la msingi ni hatua nyengine ya kuimarisha uhusiano na udugu kati ya Norway na Zanzibar.
Alisema kuwa ni dhahiri kuwa hatua hiyo ni ishara ya urafiki wa dhati walionao Norway kwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla “Ni imani yangu kuwa jengo hili litakuwa ni kielelezo cha udugu na urafiki wa kudumu kwa ndugu zetu hawa wa Norway”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itaondoa tatizo la makaazi kwa wataalamu wa Norway kwa kupata pahali pazuri pa kuishi na kuweza kufanya shughuli zao kwa utulivu na ufanisi zaidi.
“Tunathamini sana na kushukuru kwa uwamuzi wenu wa kulijenga jengo hili kwa gharama zenu na sisi tutaendelea kushirikiana nanyi kwa yale mambo tuliyopaswa kuyafanya ili kukamilisha ujenzi huu”,alisisitiza Dk. Shein.
Dk. Shein alitoa rai katika ushirikiano na uhusiano huo wa Norway na Wizara ya Aya, watilie mkazo suala la kuimarisha tafiti kwani uwezo unaonesha kuwa ndio chanzo cha maendeleo ya sekta zote hasa hiyo ya afya. Alisema kuwa nchi hiyo ilianza uhusiano katika sekta hiyo kwa kusaidia katika kuimarisha huduma za benki ya damu hapa Zanzibar.
Alieleza kufarajika kwake na ushirikiano wa Norway na Zanzibar kwenye maeneo mengi yakiwemo kuimarisha uhusiano kati ya Hospitali ya MnaziMmoja na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland ambapo tayari utekelezaji wa makubaliano umeshaanza kwa kubadilishan wataalamu.
Pia, alieleza kufarajika na utekelezaji wa mazungumzo kati yake na uongozi wa Hospitali ya Haukland ulioongozwa na Profesa Kvinsland Novemba mwaka jana, juu ya msaada wa huduma za maradhi ya figo, saratani na moyo ambapo hatua hiyo imeanza na mtaalamu wa maradhi ya figo atafika karibuni. Dk. Shein alipongeza azma ya Chuo cha Sayansi ya Afya hapa Zanzibar ya kuanzisha mafunzo ya ‘Biomedical Engineering’, yaani uhandisi wa vifaa vya hospitali.
Uongozi wa Wizara ya Afya umeeleza kuwa Norway imekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo hapa Zanzibar ambapo hivi sasa katika uhusiano na Wizara hiyo imeweza kusaidia miradi kadhaa ndani ya sekta ya afya nchini. Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema kuwa ujenzi huo umegharimu Shilingi za Kitanzania milioni 763 nalinategemewa kumaliza mwishoni wma mwaka huu.
Mamema waziri wa Afya wa Norway, Anne Grestestrom Erichsen alitoa pongezi kwa hatua za mahusiano zilizofikiwa kati ya Wizara ya Afya na Norway na kueleza kuwa hatua zote za maendeleo nchini zitaimarika kutokana na amani na utulivu uliopo.
Viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Waziri wa Afya wa Norway Mhe. Anne Crestrestom Erichsen, Mawaziri, viongozi wa vyama vya siasa na serikali pamoja na Mkuu wa Hospitali ya Haukland Profesa Steiner Kvinsland, Balozi Norway.