Hamad Rashid asema bado ni mbunge na mwanaCUF

Hamad Rashid

Na Mwandishi Wetu

IKIWA ni siku moja tangu Chama cha Wananchi (CUF) kumfukuza uwanachama Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid pamoja na wenzake watatu, mbunge huyo amejitokeza na kusema bado ni mwanachama halali wa CUF.

Rashid ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam na kusisitiza yeye bado ni mwanachama kutokana na amri iliyotolewa na Mahakama mapema juzi. Amesema kikao kilichokutana na kufanya uamuzi wa kumfukuza uanachama kilikuwa batili.

Akizungumzia tetesi za yeye na wenzake kuanzisha chama kipya cha siasa amesema anakusudia kukutana na wenzake wote na baadhi ya viongozi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Morogoro ili kuangalia kama kunasababu ya kufanya hivyo.

Akijibu suala la kukata rufaa ndani ya chama hicho kuhusu kuvuliwa uanachama wa CUF, Rashid amesema hana mpango wa kutaka rufaa ndani ya chama hicho na kwamba bado ataendelea na shauri lake mahakamani.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema uamuzi wa kumvua uanachama Rashid uliofanywa na Baraza hilo yalizingatia matakwa ya sheria vifungu namba 62(4), 62(5) na 59(8) vya Katiba ya chama hicho.
Tayari CUF imewasilisha barua rasmi ofisi za bunge kumjulisha Spika wa Bunge kutangaza Jimbo la Wawi kuwa wazi baada ya chama hicho kumvua uanachama mbunge wao na kupoteza nafasi yake.