*Afikiria kuangalia upya sheria
Na Magreth Kinabo–Maelezo, Dar es Salaam
MSAJILI wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amesema kwamba ofisi yake inafikiria kubadilisha mifumo ya uchaguzi ili kuweka utaratibu wa kulinda haki za msingi za mpiga kura pale inapotokea chama fulani kinamfukuza uanachama mbunge.
Tendwa ametoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu mara baada ya kuapishwa kwa viongozi wapya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Amesema wimbi la fukuza fukuza uanachama kwa wabunge si geni kwani liliwahi pia kutokea katika mfumo wa chama kimoja.
Tendwa alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali juu ya matukio ya vyama kuwafukuza uanachama wabunge, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid aliyefukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) na hivyo kujikuta akipoteza wadhifa wake wa ubunge.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi inapotokea hali ya namna hiyo, ipo haja ya kuangalia mpigakura anafikiriwaje na chama juu ya sifa na haki za msingi dhidi yake.
“Tunafikiria tuweze kubadilisha mifumo hiyo ya uchaguzi kwa kuangalia mbunge na lazima tumfikirie mpigakura. Lazima tuangalie hali ya uchumi,” alisema Tendwa.
Alisema kitendo hicho kinasababisha gharama kwa serikali na wadau wengine mfano taasisi yake ambayo haikutarajiwa hata katika bajeti.
Tendwa aliongeza kuwa inapotakiwa kufanyika uchaguzi mwingine zinahitajika fedha nyingi ambapo wakati fulani alisema zinaweza kufikia sh. bilioni 19, hata hivyo hazitoshi.
Aidha alisema kuwa kifedha bado kitendo hicho kililiweka taifa katika mshtuko mkubwa kwa kuwa gharama ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine ni kubwa. Alihoji kuwa maamuzi hayo yanapofanyika hawakuona fursa ya mpigakura ana haki gani ya kumtambua mbunge wake? je chama kinafaidika nini?
Alisema wataangalia kama taratibu zilifuatwa na chama ili waweze kushauri. Tendwa alisema suala hilo limekuwa ni tabia na desturi, hivyo ni jambo linapaswa kuangalia mbele ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kwa kuwa kitendo hicho si kujenga demokrasia bali ni kuwafanya wanachama kuwa na utii wa uwoga ndani ya chama.
Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo akizungumzuia suala hilo alisema kitendo hicho cha kumwondoa mbunge katikati ya muda kinaleta matatizo makubwa ndani ya vyama, hivyo alivishauri vyama kuheshimu sheria na taratibu za mtu kumaliza muda wake.
Hivi karibuni pia Chama cha NCCR – MAGEUZI kilimvua uanachama, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kwa madai ya utomvu wa nidhamu.