M/Kiti wa NEC aapa kutenda kwa sheria na Katiba

Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jaji mstaafu, Damian Lubuva kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). (Picha na Ikulu)

Na Magreth Kinabo-MAELEZO

MWENYEKITI mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema atafanya kazi katika taasisi hiyo nyeti ya umma kwa kuzingatia sheria za nchi na Katiba. Jaji Lubuva ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete katika halfa fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Nitaendeleza shughuli za tume pale walipoishia wenzangu. Nitafanya kazi kama wenzangu kwa kuangalia Katiba na Sheria bila kupendelea wadau wote wa tume,” alisema Jaji Lubuva. Aliongeza kuwa kazi atakayoanza kwa sasa ni kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kuanzia uchaguguzi uliopita hadi uchaguzi ujao wa mawaka 2015.

“Tunaomba wanachi watuamini, tupeni muda ili tufanye shughuli za tume na tuzimalize mapema kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015,” alisisitiza huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati wa uboreshaji huo utakaofanyika kabla ya uchaguzi ujao.

Rais Kikwete pia amewaapisha viongozi wengine wapya wa tume hiyo, ambao ni Makamu Mwenyekiti, Jaji mstaafu, Hamid Mahmoud Hamid na Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba. Uteuzi wa viongozi hao ulifanyika Desemba 19, 2011.

Kabla ya uteuzi huo, Lubuva alikuwa Jaji katika Mahakama ya Rufani Tanzania na baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi. Lubuva anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Lewis Makame ambaye mkataba wake wa utumishi wa umma ulifikia mwisho Julai 2011.

Wakati Hamid alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kustaafu kwake na anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Jaji Omari Makungu. Jaji Makungu aliteuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye akateuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Mallaba, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Sehemu ya Mikataba (Contracts and Treaties) katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mallaba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Rajabu Kiravu ambaye amemaliza mkataba wake wa utumishi Septemba, mwaka huu, 2011.