Hamad Rashid mwisho

Mh. Hamad Rashid

Baraza Kuu cha Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limewafukuza rasmi viongozi wanne wa chama hicho, akiwemo muasisi wake na Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohammed.

Viongozi hao wamefukuzwa baada ya kupatikana na hatia ya kula njama za kukivuruga chama hicho na kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa kitaifa kwa kuwahusisha na tuhuma za ubadhirifu wa fedha na kuzorotesha chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema viongozi hao wamepoteza nyadhifa zao zote baada ya baraza hilo kuwavua uanachama wa chama hicho.

 WALIOTIMULIWA

Aliwataja waliotimuliwa ambao pia walikuwa wajumbe wa Baraza Kuu kuwa ni Hamad Rashid Mohammed, Doyo Hassan Doyo; Shoka Khamis Shoka na Juma Said Sanani.

Hata hivyo, Yasin Mrotwa amepewa karipio kwa kwenda kinyume na maadili ya chama hicho.

“Baada ya kutafakari kwa kina maelezo ya tuhuma zao na utetezi walioutoa, Baraza Kuu la Uongozi limeridhika kuwa viongozi hao wamefanya vitendo vinavyowapotezea sifa za kuendelea kuwa wanachama,” alisema Mtatiro.

Alisema vitendo walivyofanya haviwezi kuachwa kwa sababu hata kama angekuwa mwenyekiti wa chama hicho au katibu mkuu Baraza Kuu lisingesita kuwachukulia hatua kama hiyo.

Mtatiro alisema viongozi hao wanatuhumiwa kuwakashifu viongozi kupitia vyombo vya habari kwa kuwapaka tuhuma za uongo za kuwaita wabadhirifu wa fedha na kuandaa genge la wahuni na kuwapiga.

“Bora afe mtu kulikoni kuua taasisi kama hii, ndiyo maana tumechukua maamuzi hayo kulinda katiba na heshima ya chama,” alisema.

Alisema kikao hicho kiliwapa nafasi ya kujitetea kila mtuhumiwa kwa muda wake kwa kuzingatia kifungu cha 10 (5) cha katiba ya chama hicho kabla ya kutolewa hukumu dhidi yao.

Alisema matokeo ya kuwafukuza yamezingatia pia kifungu cha 62(4) 62(5) na 54(8)(d) vya katiba ya chama hicho baada ya hoja kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema maamuzi hayo pia yalipewa uzito kwa kuzingatia kifungu cha 63(1) (j) 64 (4) 64 (5) na 64 (6), ambavyo vyote vimetoa uwezo wa kumfukuza kiongozi au mwanachama baada ya taratibu zote za kikatiba kuzingatiwa kabla ya kutolewa uamuzi huo.

Pia, alisema uamuazi wa kuwafukuza uliungwa mkono na wajumbe 45 kati ya 47 waliopiga kura ambapo wajumbe wawili kutoka Tanzania Bara walipinga kura ya hapana.

Aidha, Mtatiro, alisema Mrotwa pamoja na kupewa karipio, mwenendo wake utaendelea kuchunguzwa.

Alisema watuhumiwa wengine walikuwa wanaendelea kuhojiwa na kupewa nafasi ya kujitetea katika kikao hicho kilichokuwa kinaendelea jana usiku.

MACHANO TUACHE JAZBA

Akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, aliwataka wajumbe kujiepusha na jazba kabla ya kupitisha uwamuzi dhidi ya watuhumiwa. Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 56.

Machano aliwataka wajumbe wawe makini katika kuwajadili viongozi hao kwa kujiepusha na jazba na badala yake wawajadili kwa kuzingatia ustaarabu kabla ya kutoa maamuzi.

“Matumaini yangu ni kwamba wajumbe tutatulia katika kujadili mada iliyo mbele yetu kwa kuweka kando jazba ili kufikia maamuzi ya kistaarabu yatakayo heshimika,” alisema Machano. Alisema suala la umakini lina umuhimu katika kikao hicho kutokana na umuhimu wake.

 KAULI YA MAALIM SEIF

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif  Hamad, alisema maamuzi yatakayotolewa na kikao hicho yatakuwa halali kutokana na masharti ya idadi ya wajumbe wanaotakiwa kikatiba kukamilika.

 Alisema kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe 56 wa baraza kati ya 61, wakati masharti ya katiba yameweka wazi kuwa nusu ya wajumbe wa baraza hilo wanapohudhuria kikao kama hicho maamuzi yake yanakuwa halali na yanapaswa kuheshimiwa na vikao vya chama na wanachama wake.

 Alisema maamuzi ya kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza Kuu yalifikiwa na kamati tendaji ya Chama hicho iliyokutana Desemba 30 na 31, 2011 Zanzibar,kutokana na uwezo iliyopewa wa kikatiba kwa kuzingatia kifungu cha 62 (1) na marekebisho yake ya mwaka 2009.

 KIKAO CHACHELEWA

Kikao hicho kililazimika kuanza saa 4:00 asubuhi badala ya saa 3:00 kutokana na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania Bara kuchelewa.

BLUE GUARD

Kikao hicho kilifanyika chini ya ulinzi mkali wa askari wa Blue Guard ambao walionekana kuimarisha ulinzi kuanzia ghorofa ya kwanza ya ukumbi wa mkutano wa Mlingoti hadi chini huku wakihoji watu waliokuwa wanaingia na kutoka ndani ya hoteli ya kitalii ya Mazson.

Askari wa chama hicho walionekana wakizunguka jengo la hoteli hiyo baadhi yao wakiwa wamevaa miwani ya rangi nyeusi  ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika katika mazingira ya usalama.

Hata hivyo maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao wanamlinda Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, hawakuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi na kulazimika kubakia nje ya mlango wa mkutano na chini ya jengo la hoteli.

 “Nawaombeni waandishi wa habari muondoke baada ya kazi ya ufunguzi kukamilika, tutaonana baadaye baada ya kazi kukamilika,” alisema Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma, Salim Bimani.

Wajumbe wa Baraza Kuu walianza kuwasili majira ya saa 2:30 asubuhi wengi wao wakionekana kuwa na tabasamu wengi wao wakisalimiana na kucheka.

 Hamad aliwasili hotelini hapo majira ya saa 2: 35 akitembea mwendo wa kujiamini akiwa katika hali ya tabasamu na mchagamfu  huku akionekana kutumia muda mwingi kubadilishana mawazo na wajumbe wenzake.

Mgogoro ndani ya CUF uliibuka baada ya Hamad Rashid, kumtaka Maalim Seif kujivua wadhifa wa ukatibu mkuu ili nafasi hiyo ishikwe na mtu mwingine.

 Alisema  kutokana na Maalim Seif kushikilia nafasi zote mbili, chama kimedhoofika kutokana na uwajibikaji mdogo wa viongozi Tanzania Bara na Zanzibar.

HAMAD RASHID KUZUNGUMZA LEO HATMA YAKE

Akizungumzia hatua hiyo, Hamad alisema alitarajia kuwa Baraza Kuu lingefuata matakwa ya kiimla ya Malim Seif hivyo haki kutotendeka.

Akisema Malim Seif amekiuka amri ya mahakama iliyozuia mchakato wote wa kikao cha jana cha Baraza Kuu kufanyika.

Alisema amri ya Mahakama ilitoka jana saa 3:40 asubuhi na saa 4:45 ikafikishwa kwake na saa 6:30 alimwandikia Maalim Seif barua akimjulisha amri hiyo. Hata hivyo, alisema Maalim Seif aliupinga mchakato wote.

Alisema hakubaliani na maamuzi hayo kwa kuwa wakati yanatolewa, watuhumiwa wote walikuwa hawajamaliza kuhojiwa.

Alihoji kama Makamu wa Kwanza wa Rais haheshimu mihimili mingine ya dola maana yake ni nini.

Kuhusu hatma yake, Hamad Rashid alisema leo atazungumza na waandishi wa habari kutangaza msimamo wake.

CHANZO: NIPASHE