Magufuli awavimbia wabunge wa Dar

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli amesema hayupo tayari kushusha nauli ya kivuko cha Kigamboni kama wanavyoshinikiza baadhi ya wananchi na wanasiasa tofauti na agizo lake la awali.

Magufuli ametoa ufafanuzi huo jana alipokuwa akizungumza na wanahabari na kusisitiza kuwa serikali haiwezi kushusha nauli hiyo kwa kuwa viwango vipya vimepitishwa kialali kwa mujibu wa sheria.

Amesema lengo la kupandisha bei hiyo ni kutaka kuboresha pato la taifa na kuongeza kivuko kimoja kitakachofanya safari zake kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam ili kupunguza msongamano kwa wananchi wanaotumia barabara.

Waziri huyo amewataka wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam waliojiingiza katika sakata hilo kuacha mambo ya siasa na badala yake wafanye mambo yatakayowaletea maendeleo. Amesema anaamini mageuzi yaliofanyika ni sahihi na kama wanasiasa wanaona hayupo sahihi yupo tayari kuwakabidhi kivuko hicho waendeshe wao.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi jana imetia saini mkataba wa awamu ya pili na mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kilwa Kajima Corporation ambaye amekubali kujenga upya barabara hiyo kwa gharama zake baada ya kubainika barabara hiyo aliyojengwa mwaka 2008 haikuwa na viwango stahili.

Waziri Magufuli amesema mkandarasi ataondoa tabaka la lami katika urefu wa Kilomita 5.1 na tabaka jipya la lami lenye unene wa sentimeta 7 akitumia lami yenye kiwango cha ugumu cha 40/50 na kokoto za ukubwa wa milimita 20, ujenzi ambao utakuwa na kiwango kikubwa kiuimara.

Mkataba huo wa awamu ya pili ya wa Ujenzi wa barabara umesainiwa mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na Balozi wa Japani nchini Tanzania Masaki Okada na Waziri wa Ujenzi Dakta John Pombe Magufuli.

Balozi Masaki Okada amesema marekebisho ya barabara hiyo yatafanywa na mkandarasi wa kampuni ya Kajima toka Japan kwa gharama zao na itaimarisha tabaka la msingi la barabara kwa kuchanganya saruji katika urefu wote wa barabara hiyo.