Fidia ya Kimbangulile kwa Samata yakwama

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

*TFF yaonya usajili dirisha dogo 2011/2012

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana Desemba 30 mwaka jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samata.

Ikumbukwe kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili malipo baada ya Simba kumuuza Samata kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kimbangulile ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Uamuzi wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea timu hiyo.

Kwa upande wa solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji huyo TP Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya Kimbangulile.

Wakati huo huo; kwa upande wa Daraja la Kwanza, Kamati hiyo imetoa siku saba kwa klabu ambazo zimezidisha idadi ya wachezaji ili zipunguze, kwani kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 30.

Klabu nyingi baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo zimepitisha idadi ya wachezaji 30 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni. Hivyo kwa klabu ambayo itashindwa kupunguza wachezaji ndani ya muda huo, TFF itahesabu hadi 30 na wachezaji watakaokuwa wamezidi wataondolewa.

Kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), klabu ya Villa Squad ndiyo imekutwa na kasoro katika usajili wake ambapo imetoa kwa mkopo wachezaji wanne na imepokea wengine watano kwa mkopo.

Kwa mujibu wa kanuni ya mkopo, klabu haitakiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watano iliotoa au kuingiza kwa mkopo kwa wakati mmoja. Hivyo Villa Squad imetakiwa kuwaandikia barua za kuwaacha wachezaji wanne iliowatoa kwa mkopo ili wawe huru (free agents).

Pia Kamati imeagiza viongozi wa juu wa Majeshi ambayo yanamiliki timu za mpira wa miguu kupewa elimu ya kanuni za usajili, kwani mafunzo ya kijeshi na uhamisho wa wachezaji ambao ni askari vimekuwa vikiathiri viwango vya timu zao kwenye ligi.