RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Desemba 30, 2011, alifanya uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Mkuu na pia amefanya uhamisho wa Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, inasema kuwa, Fanuel Mbonde, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria, na Alphayo Kidata, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa, Eliakim Maswi, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini. Kabla ya uteuzi wake, Maswi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa sasa anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini. Rais Kikwete pia amemteua, Peter Ilomo, Mratibu Mkuu wa Sera na Mipango, Ofisi ya Rais, Ikulu, kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu.
Naye, Susan Paul Mlawi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi huu, Mlawi alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri (Cabinet Under Secretary) Kamati ya Katiba na Bunge ya Baraza la Mawaziri.
Taarifa ya Luhanjo inamalizia kwa kusema kuwa mabwana Maswi na Ilomo pamoja na Mlawi wataapishwa Januari 2, 2012, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.