Demba Ba achaguliwa kikosi cha Senegal

Demba ba katika moja ya mahangaiko yake uwanjani

Senegal imetaja kikosi chake imara cha wachezaji 23 kitakachoiwakilisha nchi hiyo katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, huku kikiongozwa na mpachika mabao hatari katika Ligi Kuu ya Kandanda ya England, Demba Ba.
Mfungaji hodari msimu uliopita katika Ligi ya Ufaransa Moussa Sow n mshambuliaji wa klabu ya Freiburg Papiss Demba Cisse pia wamo katika kikosi hicho.
Simba hao wa Teranga kama wanavyojulikana, pia watakuwa na mshambuliaji mwengine hatari Dame N’Doye, ambaye alichaguliwa mchezaji bora nchini Denmark mwaka huu.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya vijana ya Ufaransa Armand Traore, ambaye hivi karibuni alibadili utaifa wake kwa ajili ya kuichezea Senegal, yumo katika kikosi hicho na itakuwa mara yake ya kwanza kucheza michuano mikubwa ya Afrika.
Ni wachezaji sita tu walioiwakilisha Senegal katika michuano ya mwaka 2008 wamesalia katika kikosi hicho.
Mlinda mlango Bouna Coundoul, walinzi Bayal Sall, Souleymane Diawara, Guirane Ndaw, Pape Malickou Diakhate na mshambuliaji Mamadou Niang walikuwemo katika kikosi kilichowakilisha nchini Ghana kilichotolewa katika mzunguko wa kwanza.
N’Doye, ambaye mabao yake 25 katika mechi 31 alizochezea timu yake ya FC Copenhagen yalisaidia timu hiyo kunyakua ubingwa wa Denmark, ni miongoni mwa washambuliaji saba waliochaguliwa na kocha wa timu ya taifa ya Senagal kwa ajili ya mashindano hayo.
Senegal ipo kundi A katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika pamoja na wenyeji wenza Equatorial Guinea, Zambia na Libya.

-BBC