Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka wananchi wa Dar es Salaam wanaokaa mabondeni maeneo mbalimbali kuondoka wenyewe, kabla ya kuchukua hatua za kuzibomoa nyumba hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq amewaambia waandishi wa habari jana alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya hatari ya maeneo hayo kufuatia taarifa za kuendelea kwa mvua kubwa za vuli.
Juzi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa utabiri wa hali ya hewa na kudai vipimo vya mvua vinaonesha bado maeneo mbalimbali ya nchi ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kuwa na mvua kubwa zitakazonyesha muda wowote kuanzia sasa.
TMA katika taarifa yake imewataka wakazi wa maeneo ya mabondeni kuondoka maeneo hayo mara moja kwani huenda mvua hizo zikaleta madhara makubwa kama ilivyotokea juzi jijini Dar es Salaam kwa wakazi wa mabondeni na sehemu ambazo hujaa maji ya mvua.
Akitoa ufafanuzi Mkuu wa Mkoa amesema Serikali italazimika kuwaondoa kwa nguvu wakazi wanaogoma kuondoka mabondeni ikiwa ni pamoja na kuzibomoa nyumba zao ili kuwanusuru na maafa ya mvua zaidi.
Licha ya baadhi ya wananchi hao waishio mabondeni kuathiriwa vibaya
na mvua kubwa ilioambatana na mafuriko tayari baadhi wameanza kurudi katika maeneo yao mabondeni jambo ambalo ni hatari.
Baadhi ya wakazi hao wameonekana wakifanya usafi kwenye nyumba zao huku wakijiandaa kurudi katika makazi hayo ya hatari hasa kipindi hiki cha mvua za vuli. dev.kisakuzi.com imetembelea baadhi ya kambi ambazo zinawahifadhi waathirika hao na kukuta namba ikipungua huku wengine wakionekana kuelekea kwenye makazi yao ya awali kufanya usafi.