Kozi ya makamishna kuanza kesho

Ofisa Habari, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura

KOZI kwa ajili ya makamishna wa mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inafanyika kesho (Desemba 28 mwaka huu) na keshokutwa (Desemba 29 mwaka huu).

Kwa mujibu wa taarifa iliyo tolewa leo na TFF, washiriki wa kozi hiyo itakayofanyika ofisi za TFF ni wale wanaoomba kwa mara ya kwanza (beginners), na waliokosa ile ya awali iliyofanyika Agosti 6-8 mwaka huu. Pia ambao hawakufaulu katika kozi ya awali wanayo fursa ya kushiriki ya sasa.

Aidha taarifa imesema washiriki wanatakiwa kuwa waamuzi wastaafu na viongozi (administrators) wa mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali. Pia wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao halisi (original) vya elimu.

Kutakuwa na mitihani ya kuandika ya sheria za mpira wa miguu na picha (video clips). Kwa wanaotaka kuwa makamishna ni lazima washiriki katika kozi ambapo ada ni sh. 10,000.

Makamishna waliofaulu kwenye kozi iliyopita ni Abdallah Mitole, Amri Kiula, Arthur Mambeta, Charles Komba, Charles Ndagala, David Lugenge, Edward Hiza, Fulgence Novatus, Gabriel Gunda, George Komba, Godbless Kimaro, Hamis Kissiwa, Hamis Tika, James Mhagama, Jimmy Lengwe, Michael Bundara, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Omari Mwamela, Paul Opiyo, Pius Mashera, Salim Singano, Victor Mwandike na William Chibura.