Mkoa wa Pwani kuwakwamua vijana

Vijana 400 kutoka mkoa wa Pwani na Wilaya ya Korogwe wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo wakati akifunga mafunzo maalum yaliyoandaliwa na mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwaondoa vijana katika maeneo yanayowadhalilisha na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa na maisha bora.

Na Lydia Churi, MAELEZO-PWANI

VVIJANA nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, ikiwemo kujituma na kuacha uvivu ili waweze kujiletea maendeleo. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi Desemba 24 alipokuwa akifunga mafunzo ya siku moja ya Vijana wa Mkoa wa Pwani na wilaya ya Korogwe.

“Mabadiliko ya kijana yatatokana na uamuzi wa kijana mwenyewe katika mipangilio ya maisha yake,” alisema Waziri huyo mwenye dhamana na vijana Tanzania.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na vijana 400 wa mkoa wa Pwani na wilaya ya Korogwe (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo maalum yaliyoandaliwa na mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwaondoa vijana katika maeneo yanayowadhalilisha na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mantumu Mahiza. (Picha zote na Lydia Churi –MAELEZO)


Akizungumzia mabadiliko ya Katiba ya Tanzania, Waziri Nchimbi alisema, Katiba ya miaka 50 ijayo itawahusisha zaidi vijana wa sasa hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni wakati utakapowadia.

Akizungumzia ugonjwa wa Ukimwi, Waziri Nchimbi alisema ugonjwa huo bado ni hatari huku akidai dawa zote zinazotangazwa kutibu maradhi hayo hazina ukweli hivyo kuwataka vijana kuzungumzia kwa Uwazi na bila ya aibu njia za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo yakiwemo matumizi sahihi ya kondomu.

Aidha aliongeza kuwa taifa lijalo litawategemea sana vijana na hakutakuwa na taifa iwapo vijana wote watapotea kutokana na ugonjwa wa ukimwi. Alibainisha kuwa nchi imepoteza wataalamu wengi hivyo vijana hawana budi kuhakikisha hawapati maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema uamuzi wa kijana kuishi maisha marefu kwa kukwepa maambukizi ya virusi vya ukimwi ni wa kijana mwenyewe. Aliongeza kuwa Asilimia 90 ya maambukizi ya Ukimwi yanatokana na ngono zisizo salama na kwamba vijana ndiyo wanaoongoza kwa kutopenda kufa wakati huohuo wakipenda ngono zisizo salama jambo ambalo haliwezekani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Pwani, alisema Mkoa wake uliamua kuwakutanisha vija wapatao 400 kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani na wilaya moja ya Tanga (Korogwe) ili kuwaondoa katika maeneo yanayowadhalilisha kwa kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Alisema, mkakati wa Mkoa wake ni kuwakutanisha vijana wengi zaidi wenye umri wa kati ya miaka 18- 25 katika Kambi ya Maarifa na kuwapatia maarifa na ujuzi watakaoupenda zikiwemo stadi za kilimo cha kisasa ili waweze kujitegemea. Aliongeza kuwa mkoa wa Pwani unazo rasilimali nyingi ambazo haziwasaidii vijana, hivyo kwa kupitia kambi hizo vijana watafaidika. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi anuai wa Serikali wakiwemo Katibu Tawala Pwani, wakuu wa wilaya na baadhi ya wabunge.