Dk Shein: Tumuenzi Karume kwa vitendo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka vijana kumkumbuka Marehemu Abeid Amani Karume kwa vitendo.

Dk. Shein aliyasema hayo janna baada ya kupokea matembezi ya kumuenzi muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar marehemu, Abeid Karume katika viwanja vya Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui, mjini Zanzibar.

Matembezi hayo ambayo yamefanywa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) yalianza Aprili 3, mwaka huu eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja yaliwahusisha vijana wapatao 100 na jana yaliitimisha mzunguko wao eneo la Kisiwandui.

Katika maelezo yake, Dk. Shein ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema marehemu Karume alitembea ndani na nje ya nchi kwa kutafuta maisha yake pamoja na kutafuta uhuru wa Wazanzibar, hivyo matembezi yaliofanywa yawe na msingi huo.

“Abeid Karume alikuwa anapenda watu, anasaidia watu na alisimama imara kuhakikisha ukweli unatendeka, umoja, upendo na mshikamano…ndiyo maana alikuwa mstari wa mbele kuondoa unyonge uliokuwa umejengeka kwa Wazanzibari wanaondokana na unyonge,” alisema Dk. Shein.

Aidha Dk. Shein aliwataka vijana kuendeleza umoja, mshikamano na upendo kwani ndio jambo muhimu na la msingi katika ujenzi wa nchi na Chama Cha Mapinduzi kwa maendeleo ya wote.

Alisema kwa tendo la matembezi ya kumuenzi Abeid Amani Karume pekee vijana wanamengi ya kujifunza na endapo watafuata nyayo za kiongozi huyo watakuwa wanachama wazuri na mfano katika kukiimarisha chama.

Hata hivyo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa UVCCM kwa kushiriki vema katika matembezi hayo pamoja na viongozi wote walioyaunga mkono matembezi hayo maeneo yote yalipopita.

Awali Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Beno Malisa akimkaribisha Dk. Shein kuzungumza katika sherehe hizo alibainisha kuwa siku zote UVCCM inajitahidi kufanya mambo yake kwa kuafuata taratibu na kanuni ili kuwaenzi waasisi wa chama hicho.

“…UVCCM itaendelea kukilinda chama na kuzilinda Serikali zote mbili kwani jumuia hii iko imara na thabiti, tumeanza vizuri na moto wetu hauzimwi,” alisisitiza Malisa.

Akisoma risala ya vijana wa CCM, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Jamali Kasimu Ali alisema wanathamini na kutambua mchango mkubwa wa marehemu Karume katika kuiletea maendeleo Zanzibar.

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Fatuma Karume, Asha Balozi, Pili Balozi na viongozi wengine wa CCM, na vyama vya upinzani.