Serikali yatenga ardhi kwa wakazi wa mabondeni

Rais Jakaya Kikwete akitembelea maeneo yalioathirika na maafa ya mafuriko. Picha na Ikulu Dar.

*Vifo vyaongezeka na kufikia watu 20

Na Joachim Mushi

IKIWA ni siku moja tangu kuibuka kwa maafa makubwa ya mafuriko baada ya kunyesha mvua kubwa za siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam, iliyoleta athari kubwa kwa wananchi na kusababisha vifo.

Serikali imesema imetenga eneo maalumu lenye ukubwa wa hekari 2,000 ambalo litatumika kuwagawia viwanja wakazi wa mabondeni jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akiwafariji waathirika wa maafa hayo katika moja ya kambi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia waathirika hao, pamoja na kuyatembelea maeneo yalioathirika n maafa hayo.

Akizungumza katika Kambi ya Mchikichini Rais Kikwete amesema eneo hilo tayari limeandaliwa Wilaya ya Kinondoni na litatangazwa baada ya taratibu za kukamilika na kugawiwa wakazi hao. Aidha akiwapa pole amewataka kuwa wavumilivu na kutorejea katika makazi yao (mabondeni) kwa sasa kwani bado kuna taarifa za mvua hizo kuendelea hadi Februari 2011. Rais Kikwete pia ametangaza maafa hayo ni janga la Taifa.

Amesema Serikali itahakikisha inatoa huduma zote muhimu kwa waathirika hao kwa sasa katika kambi zilizoandaliwa, hivyo kuzitaka kamati za maafa kuhakikisha zinatekeleza jukumu hilo kwa ushirikiano.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya waathirika katika kambi kadhaa kuwa hawajapata msaada wa msingi tofauti na taarifa zinazotolewa na viongozi. dev.kisakuzi.com ilishuhudia waathirika katika Kambi ya Rutihinda iliyopo katika Shule ya Msingi Rutihinda wakilalamika kuwa hawajapatiwa msaada wowote tangu jana, huku wengine wakianza kutawanyika.

Malalamiko hayo pia yalitolewa na baadhi ya waathirika Kambi ya Mchikichini, japokuwa jitihada za Serikali na baadhi ya watu na makampuni binafsi yameanza kutoa misaada. Kampuni ya Vodacom imetoa kiasi cha sh. milioni 30 huku Mamlaka ya Bandari (TPA) ikiwa imetoa kiasi cha milioni 20.

Hata hovyo vifo vya maafa hayo vimeongezeka kutoka sh. 14 vya jana hadi kufikia 20 kwa sasa, huku wakazi takriban 4,000 wakiachwa bila makazi. Akizungumza na dev.kisakuzi.com leo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema vifo vimeongezeka na kufikia 20 mpaka sasa.

Kampuni ya Vodacom mbali na kuchangia milioni 30, imeweka utaratibu wa kuwawezesha wateja wake kuchangia fedha kwa waathirika hao kupitia M-Pesa na nambari ya Red Alert 15599 mteja anaweza kuchangia sh. 500 kwa kutuma ujumbe mfupi – SMS wenye neno MAAFA na hakuna ukomo wa ujumbe na kwa njia ya M-Pesa mteja anaweza kuchangia kuanzia sh. 1,000 na zaidi kwenda nambari 155990.