JK amteua Jaji Lubuva kuwa M/Kiti wa NEC

Jaji mstaafu, Damian Lubuva (wa kwanza kulia) siku alipokuwa akiapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Uongozi nchini.

*Ateua pia msaidizi na mtendaji wa NEC

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Jaji mstaafu, Damian Lubuva kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC).

Aidha, Rais Kikwete amemteua Jaji mstaafu, Hamid Mahmoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Julius Benedicto Mallaba kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Desemba 22, 2011 na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo mjini Dar es Salaam, imesema uteuzi wa viongozi hao umeanza tokea Desemba 19, 2011.

Kabla ya uteuzi wake, Lubuva alikuwa Jaji katika Mahakama ya Rufani Tanzania na baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi. Lubuva anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Lewis Makame ambaye mkataba wake wa utumishi wa umma ulifikia mwisho Julai, mwaka huu, 2011.

Naye Hamid alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kustaafu kwake na anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Jaji Omari Makungu. Jaji Makungu aliteuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye akateuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Naye Mallaba, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Sehemu ya Mikataba (Contracts and Treaties) katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mallaba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Rajabu Kiravu ambaye amemaliza mkataba wake wa utumishi Septemba, mwaka huu, 2011.