Mtanzania aombewa ITC Uingereza

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars ya Tanzania

*Mzambia kuichezesha Twiga Stars

CHAMA cha Mpira wa Miguu Uingereza (FA) kimetuma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) mchezaji Douglas Didas Masaburi ili ajiunge na klabu ya nchini humo.

Masaburi mwenye umri wa miaka 21 anaombewa ITC ili ajiunge na klabu ya Coventry Spartans akiwa mchezaji wa ridhaa. Coventry Spartans iko katika Ligi Daraja la Pili ya Midland.

Mchezaji huyo anaombewa ITC kutoka katika klabu ya New Rule Power. TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.

Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Zambia kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia.

Mechi ya kwanza itachezwa jijini Windhoek, Namibia kati ya Januari 13, 14 na 15 mwakani. Mwamuzi ni Gladys Lengwe wakati waamuzi wasaidizi ni Patience Mumba na Mercy Zulu.

Mwamuzi wa akiba (mezani) atakuwa Bookanang Lekgowe kutoka Botswana wakati kamishna wa mechi hiyo kutoka Afrika Kusini atakuwa Smith Hilton Fran.

Mechi ya marudiano itachezwa Januari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars inayofundishwa na kocha Charles Boniface Mkwasa akisaidiwa na Nasra Mohamed imeanza rasmi mazoezi jana (Desemba 19 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo.